Na Elizabeth Joseph,Arusha.
Waandishi wa Habari nchini wameshauriwa kuwa na uelewa mkubwa wa masuala ya Fedha za umma ikiwemo sheria na kanuni zinazosimamia matumizi ya fedha hizo.
Ushauri huo umetolewa jijini Arusha na Mwakilishi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mkaguzi Mkuu wa Nje(CEA) Mkoa wa Arusha Bw,Valance Rutakyamirwa wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha yaliyolenga kutoa elimu juu ya shughuli zinazofanywa na Ofisi ya CAG yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani humo (APC) kwa kushirikiana na Ofisi ya CAG.
Bw, Rutakyamirwa amesema kuwa ni muhimu kwa Waandishi wa Habari kuongeza uelewa mpana zaidi juu ya fedha za umma,mifumo ya bajeti pamoja na taratibu za manunuzi ili kusaidia kufanya uchunguzi bora katika uandaaji wa taarifa zao ili kuuhabarisha umma kupitia taarifa zao.
Aidha amewataka Waandishi hao kuhakikisha wanafahamu vizuri masuala mbalimbali yanayohusu ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ikiwa ni pamoja na kazi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ikiwa ni pamoja na sheria,taratibu na kanuni zinazoendesha na kusimamia ofisi hiyo.
Naye Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikali Ofisi ya CAG Bw,Focus Mauki amewataka Waandishi hao kutumia elimu waliyopewa katika mafunzo hayo kuelimisha wananchi juu ya namna mfumo wa uwajibikaji wa ofisi ya CAG unavyofanya kazi kupitia vyombo vyao vya habari.
Akifunga mafunzo hayo Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha Bw,Claud Gwandu aliishukuru ofisi ya CAG kwa mafunzo hayo kwakuwa ni yanaongeza maarifa katika utendaji kazi wao na kusaidia kutoa taarifa zilizosahihi juu ya masuala ya Ukaguzi na hesabu za Serikali.
Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo aina ya Taasisi kuu za Ukaguzi,Aina ya ripoti na taratibu za maandili za ripoti za CAG pamoja na misingi ya mawasiliano baina ya ofisi ya CAG na waandishi wa Habari.
Post A Comment: