Kampuni ya Twiga Minerals  Cooperation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Cooperation  imeongoza katika kipengele cha Kampuni zenye ubia na Serikali katika utoaji Gawio kwa Serikali.

Tuzo ya ushindi kwa kampuni  hiyo ilitolewa Agosti 19, 2023 jijini Arusha  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu na Taasisi za Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma.

Akizitaja kampuni zilizofanya vizuri katika kipengele hicho, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amesema kuwa kampuni ya Twiga imefanya vizuri katika kipengele hicho kwa kutoa gawio kwa Serikali ya kiasi cha shilingi bilioni 84 Mwaka wa Fedha 2022/23.

Kampuni ya Barrick ndiyo kampuni ya kwanza kuingia ubia na Serikali miongoni mwa kampuni za madini hali ambayo ilihamasisha na kampuni nyingine kutoka nje kusaini mikataba yenye thamani kubwa  na Serikali katika shughuli za uchimbaji wa madini ya aina mbaimbali yakiwemo madini muhimu na ya mkakati.

Aidha, ubia na kampuni hiyo  umetajwa mara kadhaa kuwa  mfano wa kuigwa  na mataifa mbalimbali huku kampuni hiyo   ikitaja kuutumia ubia wa Tanzania kuutekeleza katika nchi nyingine ilikowekeza.

Migodi iliyo chini ya kampuni ya Twiga Minerals ni pamoja na North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi. 

Mwezi Januari, 2023 wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Meneja Mkazi wa kampuni ya Twiga Melkiory Ngido alisema  mwaka 2020 kampuni hiyo ilitoa gawio kwa Serikali kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 huku kipindi cha mwaka 2017 hadi 2022 kiasi cha shilingi bilioni 24.3 kilitolewa kwa halmashauri kama tozo mbalimbali zinazotozwa katika maeneo yenye shughuli za migodi yake.

" Kampuni ya Twiga imepanga kuendeleza  shughuli za utafiti ili kuongeza uhai wa migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu na ni matazamio ya uhai wa mgodi wa Bulyanhulu ni kufika mwaka 2040 na North Mara kufika mwaka 2039," alisema  Ngido katika kikao hicho.

Share To:

Post A Comment: