Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha nyumba zinazojengwa zinakidhi mahitaji ya soko kwa miaka mingi ijayo ikiwemo ubora wa nyumba hiyo na sehemu za kupata mahitaji.

Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kufungua Jengo la Makazi la Kibiashara la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) lililopo katika eneo la Sekei Jijini Arusha, Jengo lililogharimu shilingi bilioni 6.86.

 Amewahimiza TBA kuzingatia tija na viwango katika miradi mingine kama ilivyofanyika katika jengo hilo pamoja na kuwasihi kutekeleza kikamilifu Mpango Mkakati wa Wakala wa Majengo wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 ili kutimiza mahitaji ya makazi bora kwa Watumishi wa Umma na wananchi kwa ujumla. Amesema kukamilika kwa miradi mingi ya nyumba kutawezesha TBA kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewaagiza TBA kuhifadhi na kutunza mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yote inapotekelezwa miradi ya ujenzi wa nyumba ikiwemo uwekaji wa miundombinu sahihi ya ukusanyaji takangumu ili kuwezesha ukusanyaji na utupaji wake. 

Amesema kila inapowezekana TBA ihakikishe inaweka miundombinu ya kuvuna maji ya mvua kwa matumizi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji wa miti na maua.

Makamu wa Rais ametoa rai kwa wapangaji wanaotumia nyumba hizo kuzingatia masharti ya mkataba wa upangishaji kwa kulipa kodi kwa wakati ili kuepukana na usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na teknolojia mpya ya uwekaji vitasa janja (Smart locks) ambavyo hujifunga pindi mpangaji anapofanya ulimbikizaji wa kodi.

 Pia amewasihi wapangaji kutunza nyumba hizo ili zibaki katika hali ya ubora kwa muda mrefu.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa adhimu ya kushirikiana na TBA katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba nchi nzima kwa kuwa Serikali tayari imeiruhusu TBA kushirikiana na Sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa ubia. 


Aidha amewasihi TBA kuendelea na mpango wa kuyaendeleza maeneo yote yaliyorejeshwa Serikalini kwa kujenga majengo ya ghorofa kama ilivyoelekezwa kwenye Ibara ya 55(h)(ii) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2020.

Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa mkoa wa Arusha kutunza mazingira kwa kuepukana na tabia ya kutupa taka ovyo kwani jambo hilo litaleta athari katika masuala ya utalii mkoani humo.

 Amewaagiza viongozi wa mkoa huo kusimamia suala hilo kwa kuhakikisha usafi unafanyika katika maeneo yote na kudhibiti utupaji taka ovyo hususani chupa za maji.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameishukuru serikali kwa kuendelea kuiamini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inayotekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi wa nyumba na majengo ya serikali katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Prof Mbarawa amesema kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo kutasaidia upatikanaji wa makazi ya uhakika kwa wakazi wa jiji la Arusha. Ameongeza kwamba mradi huo umesaidia wataalamu wazawa wa fani za ujenzi kujengewa uwezo wa taaluma kwa vitendo pamoja na kusaidia kuendelea kukua kwa kasi kwa jiji la Arusha, kuongezeka kwa mapato ya serikali pamoja na huduma za kijamii katika jiji hilo.

Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro amesema Chimbuko la mradi huo ni katika kuiwezesha Wakala kuwa na uwezo wa kujiendesha kupitia vyanzo vyake vya mapato na kupunguza utegemezi kwa Serikali. Ameongeza kwamba mapato yatakayopatikana kwenye miradi kama hiyo yatatumika kujenga nyumba nyingine za watumishi wa umma.

Arch. Kondoro ameongeza kwamba pamoja na mradi huo, Wakala wa Majengo Tanzania unaendelea kutekeleza miradi mingine kwa fedha za ndani ikiwemo Ujenzi wa Majengo ya Makazi eneo la Canadian Village, Masaki, Dar es Salaam ambapo jengo moja lenye uwezo wa kuchukua familia 12 limekamilika na majengo mengine mawili utekelezaji wake umefika asimilia 35. Wakala pia umeanza ujenzi wa Jengo la Makazi eneo la Ghana Kota jijini Mwanza ambalo utekelezaji wake umefikia asilimia 12.

Ujenzi wa Jengo hilo lenye uwezo wa kuhudumia familia 22 umeleta faida mbalimbali ikiwemo kutoa ajira kwa wataalam wa ujenzi, mafundi, vibarua, baba na mama lishe ambapo ajira zipatazo 171 zilipatikana hadi kukamilika kwa mradi huo. Mradhi huo unatarajia Kuongeza mapato ya ndani kwa Wakala kupitia kodi ya pango itakayokusanywa kwa makadirio ya Shilingi milioni mia mbili na kumi (210,000,000.00) kwa mwaka.






Share To:

Post A Comment: