IMG-20230802-WA0002


Na: James Mwanamyoto (OR-TAMISEMI)

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kujenga barabara mpya yenye urefu wa kilomita 13.8 katika Mji wa Mwanga itakayowawezesha wananchi kufika eneo lililokuwa halifikiki kwa urahisi.

Mhe. Ndejembi ametoa pongezi hizo akiwa Wilayani Mwanga wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu na barabara inayotekelezwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kupitia miradi ya BOOST, SEQUIP, GPE LANES pamoja na TARURA.

Mhe. Ndejembi amesema TARURA imefanya na inaendelea kufanya kazi kubwa katika ujenzi wa barabara hiyo na kuongeza kuwa, imetekeleza kwa vitendo kaulimbiu yake isemayo ‘kukufungulia njia kufika kusiko fikika’ kwani itawawezesha wananchi wa Mwanga kufika eneo lililokuwa ni changamoto kufikika.

Aidha, Mhe. Ndejembi amtaka Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Mhandisi David Msechu kuhakikisha anasimamia vizuri matumizi ya fedha za ujenzi wa barabara hiyo ili kusitokee mtu yeyote atakeyekwamisha jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu hiyo.

 “Tunataka ijengwe barabara yenye viwango ambayo itakayodumu kwa muda mrefu ili iwe na tija kwa wananchi na maendeleo ya taifa na ndio maana Serikali inahimiza matumizi ya teknolojia mpya ili barabara hiyo ikikamilika idumu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mwanga Mhandisi David Msechu amesema, gharama ya mradi huo kwa awamu ya kwanza ni bilioni 4.99 ambazo zitawezesha ujenzi wa madaraja 16 na kufungua kipande kilichokuwa hakipitiki.  

Mhandisi Msechu amefafanua kuwa, lengo la mradi huo ni kuimarisha miundombinu ya barabara ili kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji na kuongeza kuwa, ukikamilika utakuza mji wa mwanga, kupunguza msongamano wa magari pamoja na kuwezesha huduma za kijamii zikiwemo za afya na elimu.

 “Utekelezaji wa mradi huu ulianza Januari 04, 2023 na unatarajiwa kukamilika Januari 04, 2024 kwa mujibu wa mkataba na mpaka sasa mkandarasi amefikia asilimia 45 ya ujenzi na ameshalipwa milioni 829,” Mhandisi Msechu amefafanua.

Naye, Mbunge wa Mwanga Mhe. Joseph Tadayo amesema ujenzi wa mradi huo wa barabara ni wa kimkakati hivyo anatamani ukamilike kwa wakati ili kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji kwani jirani na eneo hilo pia kuna ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ambao ukikamilika utaongeza uhitaji wa matumizi ya barabara hiyo.
IMG-20230802-WA0004
IMG-20230802-WA0006
IMG-20230802-WA0007

IMG-20230802-WA0005

IMG-20230802-WA0003
IMG-20230802-WA0008
Share To:

Post A Comment: