Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele Programu ya Korosho,Kitengo cha Udhibiti wa Visumbufu vya Wadudu waharibifu na Magonjwa, Bobnoel Assenga (kushoto) akitoa maelezo ya Wadudu waharibifu na Magonjwa kwa mkulima Cathbert Richard (kulia) aliyetembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya NaneNane 2023 yanayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi. Katikati ni Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano wa taasisi hiyo.
.....................................................
Dotto Mwaibale na Godwin Myovela, Lindi
KITUO cha Utafiti
wa Kilimo TARI Naliendele kilichopo
mkoani Mtwara kimekuwa kivutio kikubwa katika Maonesho ya Nanenane 2023
Kanda ya Kusini yanayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Katika Maonesho
hayo kituo hicho kinatarajia kuonesha teknolojia za kilimo za kuvutia wakulima
kutoka Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi ambao wameombwa kujitokeza kwa wingi
kufika katika viwanja hivyo kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo hicho Dk. Fortunus
Kapinga kuhusu maonesho hayo Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni
Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mawasiliano alisema wamejipanga vizuri na
kuwa wakulima wategemee kupata ujuzi mkubwa wa masuala ya kilimo katika
maonesho hayo.
Alisema TARI
Naliendele ni miongoni mwa vituo 17 vilivyopo chini ya Taasisi ya Utafiti wa
Kilimo Tanzania ambapo pia wanavituo vingine kama hivyo katika kanda zingine
nchini na kueleza kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha teknolojia zinawafikia
wakulima.
Alisema TARI Naliendele wamepewa jukumu la
kitaifa la kutafiti zao la korosho, ufuta na karanga na kuwa changamoto zote
zinazojitokeza kwenye mazao hayo wao ndio wanaowajibika kutoa majibu.
Kidunda alisema
pia wamekuwa wakifanya utafiti wa mazao mengine kwa kushirikiana na vituo
vingine vilivyopewa mamlaka kitaifa na kuwa katika maonesho hayo wana programu
ya utafiti wa mazao ya nafaka, mikunde, jamii ya mizizi, mbogamboga na matunda.
Alisema mwaka huu wamejipanga vilivyo kuonesha
teknolojia zote za kilimo na litakuwa ni tukio la aina yake kwani kwa wale
waliozoea kufika kwenye siku za nanenane sasa wataona shughuli endelevu za
kituo hicho na kuwa wamefanya maboresho lukuki ya kisayansi katika kila idara.
" Kituo cha
Ngongo sio kwa ajili ya Nanenane tu bali kipo kwa mwaka mzima kueneza
teknolojia za kilimo na wataweza kuangalia teknolojia mbalimbali za korosho,
mbegu za mafuta, mikungu ya ndizi ya aina Mtwike , jamii ya mikunde na nafaka.
Mbali ya hayo pia kutakuwa na shughuli ya kuangalia jinsi ya kuongeza thamani
ya zao la korosho, ufuta na zao la karanga ambapo katika zao la korosho watu
walizoea kuja na kutafuna korosho lakini sasa watakuja kula na kunywa korosho
kwani watakuwa na juisi, jamu na mvinyo zilizotokana na zao hilo" alisema Kidunda.
Alisema katika
maonesho hayo watakuwa na kituo chao cha kanda ambacho kitatumika kutoa mafunzo
kwa wakulima hivyo wadau mbalimbali wameombwa wafike kwani wataona mengi kwenye
zao la korosho, ufuta, karanga, mihogo, viazi vitamu, kunde, choroko, mbaazi,
mahindi, uwele na mengineyo.
Alisema mazao yote
ambayo yanalimwa kwenye mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi na hata yale ambayo
hayalimwi katika mikoa hiyo lakini yanaweza kustawi maeneo hayo yatakuwepo
katika maonesho hayo.
Kidunda alisema
katika kituo chao cha Naliendele wamekuwa hawana msimu pale wameweka teknolojia
ambazo zinaonekana kwa mwaka mzima kwa ajili ya wakulima kujifunza hatua
mbalimbali za ukuaji wa zao husika kuanzia likiwa kwenye kitalu, shambani, utumiaji wa viatilifu, udhibiti wa
magonjwa na uvunaji wake.
" Tukisema
mkulima au mdau aje wakati wa wiki ya Nanenane tu kuna hatua nyingi hawezi
kuzielewa na ndio maana tunasema hatufungi maonesho haya tupo kipindi chote cha
mwaka mzima." alisema Kidunda.
Alisema TARI
imekuwa ikisogeza huduma zake kwa wananchi nchi nzima ili ziwafikie walengwa.
Alisema zamani zao
la korosho lilikuwa likilimwa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani
lakini sasa linalimwa karibu mikoa zaidi ya 20 kama Morogoro, Dodoma, Singida,
Kigoma, Tabora, Shinyanga, Katavi, Mbeya, Rukwa, Iringa, Njombe, Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo ya Same.
Alisema
kinachosemwa korosho ilimwe wapi sio mipaka ya kiutawala bali ni mahitaji ya
kiikolojia.
Kidunda alitumia
nafasi hiyo kuwaomba wakulima na wadau mbalimbali kufika kwenye maonesho hayo
ya Kanda ya Kusini yanayofanyika Ngongo mkoani Lindi kuanzia Agosti 1,2023
kwenda kujifunza teknolojia za kilimo ambayo yatafikia tamati Agosti 8, 2023.
Kidunda alisema
akiwa kama Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano jukumu lake kubwa ni
kuhakikisha teknolojia zinawafikia wakulima.
"TARI Naliendele
tunafanya utafiti na ukishafanywa kazi yetu ni kutoa matokeo ya utafiti huo na
idara yangu kazi yake kubwa ni kuuchambua na kuchakata taarifa za utafiti huo
na kuziweka katika lugha nyepesi ambayo inaweza kuwa rahisi kwa wakulima na
wadau wengine kuielewa" alisema Kidunda.
Kidunda alisema
kauli mbiu ya maonesho hayo mwaka huu ni Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa
Mifumo Endelevu ya Chakula.
Mtafiti kutoka TARI Naliendele Programu ya Korosho,
Kitengo
cha Udhibiti wa Visumbufu vya Wadudu waharibifu na Magonjwa, Bobnoel Assenga
alisema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wakulima namna ya kudhibiti visumbufu vya wadudu waharibifu na magonjwa, ikiwemo
ugonjwa wa Ubwiriunga, ugonjwa wa Blaiti na Debeki ambayo kwa kiasi kikubwa
yamekuwa ni changamoto kwa ustawi wa zao la korosho ndani ya Mikoa ya Mtwara,
Lindi na Ruvuma na kwingineko
nchini.
Alisema Tari Naliendele imekuwa ikikabiliana na kukithiri kwa wadudu waharibifu wa zao hilo wakiwemo Mbu wa Mikorosho, Mbu wa Minazi na Vidung’ata ambao ni kikwazo kikubwa cha ukuaji mzuri wa zao la Korosho ambalo linatajwa kuwa ni zao lenye uchumi mkubwa na soko la uhakika.
Assenga alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakulima kufika katika banda la TARI kwa ajili ya kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo.
Maelezo yakitolewa kwa wakulima waliotembelea banda la TARI.Afisa Kilimi Msadizi wa TARI Naliendele, Justina Misungwi, akiwapa watoto juisi iliyotengenezwa kwa zao la korosho walipotembelea banda la taasisi hiyo.
Wakulima Ahmadi Mnenele (kushoto) na Mathayo Milanzi (kulia) wakiangalia ndizi aina ya Mtwike ambayo imetokana na utafiti uliofanywa na TARI na kuleta tija. Katika ni Mtafiti wa Kilimo kutoka TARI, Zamira Matumbo.
Muonekano wa Jengo la TARI katika Maonesho hayo.
Afisa Kilimo Msaidizi, Noel Mwigune (kulia) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi, Jitulize ambao walitembelea kuona mazao ya nafaka yaliyofanyiwa utafiti na TARI.
Muonekano wa shamba la mbogamboga katika maonesho hayo.
Mtafiti Msaidizi wa Kilimo kutoka TARI, Dickson Malulu (kulia) akitoa maelezo ya kilimo cha kebichi kwa wakulima Calvin Michael (kushoto) na Evarist Eprahim waliotembelea shamba hiloMtafiti wa zao la ufuta kutoka TARI, Mohamed Fadhil, akitoa maelekezo lwa wakulima kutoka Wilaya ya Nachingwea kuhusu kilimo cha zao hilo.
Muonekano wa zao la ufuta aina ya Ziada katika maonesho hayo.
Muonekano wa zao la Muhogo aina ya Kiloba katika maonesho hayo.
Post A Comment: