Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na TARURA imeendelea kuwabana wakandarasi wanaotekeleza miradi chini ya kiwango.

Hayo yamebainishwa leo Alhamis Agosti 24,2023 na kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Bi. Mwamba Masanja wakati akitoa taarifa ya utekelezaji kazi ya robo ya Nne ya Mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema taasisi hiyo ilibaini ucheleweshaji wa ukamilishaji wa miradi ukiwemo  mkataba namba AE/001/2022/2023/SHY/W/16 unaohusisha  matengenezo ya mara kwa mara, matengenezo ya kawaida na uboreshaji wa vipande vya barabara unaotekelezwa katika kata ya Chamaguha, Ngokolo, Ndembezi, Kambarage na Mwasele chini ya usimamizi wa TARURA Wilaya ya Shinyanga.

“Tulibaini ucheleweshaji wa ukamilishaji wa mradi mkataba Na. AE/001/2022 – 2023/ SHY/W/16 wa matengenezo ya mara kwa mara (Periodic Maintenance), matengenezo ya kawaida (routine maintenance) na uboreshaji wa vipande vya barabara (Spot improvement) unaotekelezwa katika kata ya Chamaguha, Ngokolo, Ndembezi, Kambarage na Mwasele chini ya usimamizi wa TARURA Wilaya ya Shinyanga wenye thamani ya Shilingi milioni 236,606,000.00/=”

“Mradi huo unahusisha kazi kuu za uchongaji wa barabara, kuweka vifusi na kushindilia na kuchonga mitaro mradi ulitakiwa kukamilika 27.4.2023  lakini haukukamilika kwa wakati mbali ya mkandarasi kuongezewa muda wa ziada wa siku 75 kuanzia tarehe 28/04/2023 hadi 12/07/2023 kukamilisha kazi hiyo, hivyo kwa sasa mkandarasi huyo kwenye kipindi cha makato ya fedha ikiwa ni adhabu ya kuchelewesha mradi kwa mujibu wa mkataba.”amesema Mwamba Masanja

“Mbali na ucheleweshaji wa ukamilishaji wa mradi mkandarasi aliyekuwa akitekeleza mradi huo ni Brampem Global Investment. Co. L. T. D wa Shinyanga, ametekeleza kazi ya mradi chini ya kiwango kinyume na standard specification of Roads Works – 2000 ambayo ni sehemu ya mkataba wa kazi husika”.

“Baadhi ya mapungufu  katika matengenezo ya barabara nikutokuchonga barabara kwa usahihi, kina cha tabaka la kifusi kinachowekwa kitofikia kiwango kinachotakiwa  na kutosindiliwa ipasavyo na uchongaji wa mitaro ya pembezoni mwa barabara isiyoridhisha”.amesema Mwamba Masanja

“TAKUKURU ilimshauri msimamizi wa mradi ambaye ni TARURA imtake mkandarasi arudie kazi zote alizotekeleza chini ya kiwango ili thamani ya fedha iweze kuonekana”.amesema Mwamba Masanja

Ameitaja miradi mingine iliyofuatiliwa kwa inahusisha sekta mbalimbali ikiwemo elimu ambapo amesema jumla ya miradi 17 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.6 imefuatiliwa.

“Tumefuatilia miradi mingine ya maendeleo katika sekta ya elimu, afya, maji, kilimo na ujenzi ambapo jumla ya miradi ya maendeleo 17 inayotekelezwa yenye thamani ya shilingi bilioni 5.7(5,601,349,020/=) imefuatilia. Dosari ndogo ndogo zilibainika kwenye miradi miwili na ushauri ulitolewa wa kutatua dosari hizo”.amesema Mwamba Masanja

Katika kipindi hicho TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga ilipokea taarifa 35 za malalamiko ambapo 26 kati yake zinahusu rushwa huku taarifa tisa hazihusiani na rushwa na kwamba uchunguzi wake unaendelea.

Kaimu mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Bi. Mwamba Masanja amesema katika kipindi hiki kesi 11 zinaendelea mahakamani ambapo kesi mpya ni tatu na kati ya hizo kesi mbili ziliamuliwa na jamhuri ilishinda huku akitoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuhakikisha miradi yote inayoendelea kutekelezwa inakamilika kwa ubora.

Kwa mwananchi yoyote atakayeona vitendo vinavyoashiria ubadhilifu wa fedha za miradi atoe taarifa TAKUKURU kwa kufiki ofisi zetu zilizopo mtaa wa uzunguni mkabala na nyumba za bodo ya pamba au piga simu namba 0738150196 au 0738150197, ofisi ya Kahama simu 0738150198 na ofisi ya Kishapu simu 0738150199 au piga simu bure 113”.

Aidha kaimu mkuu wa TAKUKURU amesema ofisi hiyo imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu ya masuala ya rushwa inatolewa katika taasisi za serikali, binafsi na kwa wananchi kwa lengo la kuongeza wigo wa mapambano dhidi ya rushwa, ambapo pia amesema njia mbalimbali zimetumika kuelimisha kwa kipindi hicho ikiwemo uelimishaji wa klabu za wapinga rushwa 22, mikutano ya hadhara 5, semina 7 na vipindi vya Redio 4.

Pia amesema ofisi hiyo inaendelea kutekeleza program ya TAKUKURU RAFIKI ambapo ameeleza kufanyika kwa vikao vya utambuzi wa kero katika kata kumi na moja ambazo ni kata ya Pandagichiza, Lyabusalu, Ndembezi, Bulige, Ukenyenge, Shagihilu, Bunambiyu, Igaga, Busagi, Bugarama  pamoja na kata ya Mjini Shinyanga.

Katika hatua nyingine TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imejiwekea mikakati mbalimbali ya utendaji kazi kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2023 ikiwemo kufanya vikao vya kurudisha marejesho kwa wananchi kuhusu kero zilizopata majibu kutoka kwa wadau na watoa huduma ili kukabili au kuzuia rushwa katika utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Share To:

Misalaba

Post A Comment: