Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeibuka kidedea kwa upande wa Mashindano ya Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati na Mshindi wa Pili wa Jumla katika Maonesho ya 30 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki mjini Morogoro.
Ushindi huo umetangazwa Agosti 8, 2023 wakati wa kufungwa kwa Maonesho hayo ambapo Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba alitoa zawadi ya vikombe viwili kwa Chuo hicho.
Akizungumzia ushindi huo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Maulid Mwatawala amesema SUA ilikuwa na haki na kila sababu ya kupata ushindi huo kutokana na jinsi walivyojipanga pamoja huduma na Teknolojia walizokuwa wakionesha katika mabanda yao.
“Nikizungumzia ushindi wa kwanza wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati ilikuwa ni wazi tupate ushindi huo kutokana na ukubwa wetu tulio nao tusingeweza kushindanishwa na Vyuo vilivyokuwepo, lakini katika ule ushindi wa jumla tumechukua nafasi ya pili ambao nao naamini kwa aliyetushinda ameshinda kwa nafasi ndogo mno kwa sababu ya uwezo tulionao, Teknolojia tulizokuwa nazo, watu tulio nao na elimu tuliyotoa kwa wananchi”, amesema Prof. Mwatawala.
Akielezea siri ya ushindi huo Prof. Mwatawala amesema SUA kwa mwaka huu imekuja na Teknolojia ya Maabara inayotembea Maalum kwa ajili ya kutotoreshea Vifaranga, Maabara inayotembea ambayo inasaidia sana pale kunapokuwa na mlipuko wa magonjwa ya binadamu na wanyama hasa kwa zile sehemu zisizofikika kwa urahisi.
“kumekuwa na kivutio kikubwa kwa Panya wanaotambua magonjwa kama Kifua Kikuu na Majanga kwa mfano majumba yanapoporomoka kwa matetemeko panya hawa wanaweza kugundua watu waliofukiwa na kifusi lakini Maabara zetu kubwa mbili ya Afya ya Jamii na Afya ya Udongo , Hospitali yetu ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama, lakini niseme tu kwa ujumla bidhaa zote zilizooneshwa zilikuwa ni kivutio kwa wananchi”, amesema Prof. Mwatawala.
Katika hatua nyingine Prof. Mwatawala amekipongeza Kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha SUA kwa kazi kubwa ya kuhabarisha Umma kuhusu mambo yote yaliyokuwa yakiendelea katika banda hilo la SUA.
Katika ushindi huo wa jumla Bodi ya Sukari ilikuwa ya kwanza huku mshindi wa tatu akiwa ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakati kwa upande wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati nafasi ya pili ilikwenda kwa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo LITA Morogoro huku washindi wa tatu wakiwa ni Chuo cha Mafunzo ya Ufundi VETA Morogoro.
Post A Comment: