Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga imewasisitiza wanafunzi kuepuka vishawishi ambavyo husababisha ukatili, wawapo shuleni na katika jamii.

Hayo yamebainishwa na viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga wakati wakitoa elimu ya ukatili kwa wanafunzi wa shule ya msingi Bugweto kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga.

Wamewasihi wanafunzi hao kuepuka vishawishi vibaya  ikiwemo kupewa zawadi ama kununuliwa vitu mbalimbali na watu wasiowafahamu na kwamba hatua hiyo itawasaidia kuepuka ukatili, mimba na ndoa za utotoni.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti idara ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Solomon Nalinga Najulwa pamoja na mambo mengine amewasisitiza wanafunzi wa shule ya msingi Bugweto kuepuka makundi ya watu wasiofaa ambao wanajihusisha na uvutaji wa madawa ya kulevya pamoja na vitendo vya uhalifu.

Mwenyekiti idara ya wanawake na watoto SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mwinjilisti Esther Emmanuel amewasisitiza wanafunzi hao kujiepusha na vishavishi mbalimbali wanavyokutana navyo ili waweze kutimiza malengo yao na kwamba hatua hiyo itawasaidia kuwa salama katika maisha yao ya kila siku.

“Ili uwe salama kaa mbali na mtu anayekupa zawadi usiyemjua, watoto wa kike wanapewa zawadi mtu anakwambia naona unanjaa njoo nikununulie chakula njoo nikupe soda mwambie nyumbani nitazikuta mezani hata kama huna uhakika wa chakula nyumbani, kataa zawadi unayopewa bila kujua makusudi ya ile zawadi kwani zawadi hiyo ni malengo ya kukuvuta usogee ili akufanyie ukatili bila wewe kujua”.amesema Mwinjilisti Esther

Kwa upande wake katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Daniel Kapaya amewasisitiza wanafunzi wa shule ya msingi Bugweto kupaza sauti juu ya ukatatili huku akiwataka kujiepuka na tamaa ya pesa ambapo amesema hatua hiyo itawasidia kujiepusha na vitendo vya ukatili.

“Wapo baadhi ya wanafunzi mnafanyiwa ukatili lakini hamsemi mnanyamaza tu kuanzia leo msiwe na siri mtu yoyote akikupa hela humjua zikatae usiwe na tamaa ya pesa lakini pia mjitahidi kuwasikiliza walimu shuleni, wazazi lakini pia wapeni taarifa mtakapoona viashiria vya ukatili, unaweza pia kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa au tujulishe sisi SMAUJATA tutakusaidia au piga namba ya bure 116 utapata msaada usikubali wewe au rafiki yako kufanyiwa ukatili”.amesema Katibu Bwana Kapaya

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Bugweto amesema watahakikisha wanazingatia maelezo yaliyotolewa na viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga.

Naye Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugweto Yusuph  John Mbundi amewapongeza viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kwa kutoa elimu ya ukatili ambapo pia ameishukuru serikali kupitia wizara ya maendeleo ya jamii jinsia, wanawake na makundi maalum ambayo inaongozwa na Waziri Dkt. Dorothy Gwajima.

Mwenyekiti idara ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Solomon Nalinga Najulwa akitoa elimu ya ukatili kwa wanafunzi katika shule ya msingi Bugweto kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga.

 




Share To:

Misalaba

Post A Comment: