Shujaa wa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania| SMAUJATA | Kata ya Manyoni mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhi vifaa vya shule kwa watoto wawili wa kiume wanaoishi eneo la Tambukareli ambao walishindwa kupata fursa ya kwenda shuleni kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo.
.......................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania
| SMAUJATA | Kata ya Manyoni mkoani Singida wametoa msaada wa kuwanunulia
vifaa vya shule watoto wawili wa kiume wanaoishi eneo la Tambukareli ambao
walishindwa kupata fursa ya kwenda shuleni kutokana na wazazi wao kutokuwa na
uwezo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo hivi karibuni Makamu Mwenyekiti
wa Smaujata Kata ya Manyoni Wallace Shechambo alisema kazi kubwa ya Smaujata ni
kupinga ukatili wa aina zote na moja ya ukatili huo ni mtoto kunyimwa haki ya
kupelekwa shule.
'' Haki ya mtoto kupelekwa shule ni ya msingi tulipobaini kuwepo kwa watoto
hao ambao wamekosa fursa hiyo timu ya Smaujata katika kata yetu tulikutana na
kuamua kila mmoja wetu kutoa alichonacho ili kuwasaidia watoto hao ambao hivi
sasa wameanza masomo Shule ya Msingi ya Tambukareli,'' alisema Shechambo.
Shechambo alisema jukumu la kuhakikishga watoto wanapata haki yao ya kupata
elimu na mahitaji mengine ya muhimu ni la wazazi na walezi na kama watakuwa na
changamoto za kushindwa kuwapeka shuleni wanatakiwa kuwasiliana na vyombo vingine
ili waweze kupata msaada badala ya kuwaacha tu nyumbani jambo ambalo ni
kuwanyima haki hiyo ya msingi.
Alisema wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto hao wanakwenda
shuleni na kumaliza elimu ya msingi na sekondari na kuwa Smaujata watakuwa
wakiwafuatilia kwa karibu kujua maendeleo yao.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwembeni na Mshauri wa Smaujata wa kata
hiyo, Saluthary Naaly alisema baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa watoto hao
waliguswa na jambo hilo na kutokana na umoja na ushirikiano walionao walinunua
vifaa mbalimbali vya shule kama, madaftari, soksi, kalamu, vifutio, sare za
shule, nguo za kuvaa nyumbani na vitu
Hvingine na kuwapekea.
Aliwataja watoto hao kuwa ni Amosi Philipo |13| na Solomon David |9| ambao
wameonesha furaha ya kuanza shule kwani tangu wazaliwe walikuwa hawajawahi
kwenda shule.
Mjumbe wa Smaujata wa kata hiyo,
Juma Mtundu alisema walezi na wazazi ndio wenye jukumu la kuhakikisha
watoto wao wanakwenda shuleni wala sio la mtu mwingine ambapo alitoa wito
kuzingatia jambo hilo.
Mama mzazi wa watoto hao Martha Daud alisema alishindwa kuwapeleka watoto
hao shuleni kwa wakati kutokana na changamoto mbalimbali na alitumia nafasi
hiyo kuwashukuru Smaujata Kata ya Manyoni kwa hatua walioichukua ya kuisaidia
familia hiyo.
Mashujaa wa Smaujata wa kata hiyo ambao wamefanya kitendo hicho cha
kizalendo na kibinadamu cha kuwasaaidia
watoto hao na kuhakikisha wanapata elimu ya msingi ni Mwenyekiti wa Smaujata
Kata ya Manyoni, Hussein Hery, Makamu Mwenyekiti, Wallace Shechambo, Neema Masabuni,
Zena Salim, Joyce Petro, Juma Mtundu,
Henry Mallya, Juma Maiki, Mwajuma Hamisi, Sarah Omari, Agatha Evance, Gervas Siro
na Ramadhan Ngoi . |
Post A Comment: