Na John Walter-Manyara
Serikali ipo mbioni kuondoa Changamoto ya mawasiliano ya simu za mkononi mkoani Manyara kwa kujenga minara ya kisasa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, Daniel Sillo wakati alipokuwa akijibu maswali ya wananchi wa kata ya Ufana na Qameyu kuhusu huduma ya mawasiliano ya simu alipofanya ziara agosti 10,2023.
Sillo amesema kata sita zikiwemo za Secheda, Ufana na Qameyu zitapata minara ya kisasa itakayowezesha kupatikana kwa mawasiliano katika mitandao yote pamoja na Intaneti.
Amesema kuwa serikali ilishasaini mkataba na kampuni itakayofanya kazi ya kuifunga minara hiyo tangu mwezi Mei mwaka huu na kwamba makubaliano ni kukamilisha kazi baada ya miezi kumi tangu kusainiwa kwa mkataba.
Wananchi wa Kata ya Ufana na Qameyu Wilaya ya Babati wamemwambia Mbunge wao kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mawasiliano ya simu za mkononi kutokana na kukosekana kwa minara maeneo yao.
Baadhi ya wananchi hao wakizungumza na kituo hiki, wamesema kuwa wanalazimika kutafuta sehemu za miinuko au kupanda kwenye miti ili kuwasiliana hivyo wameiomba Serikali na wadau wa mawasiliano kuwasidia kujenga minara.
"Katika Kijiji chetu ni mtandao wa Halaotel pekee ndo unakubali na sio wote tunatumia Halotel,tunaomba serikali iturahisishie kupatikana kwa huduma hiyo kwani dunia ya sasa mambo yamebadilika,bila mawasiliano ni ngumu" alisema Restuta Daniel mkazi wa Ufana
Nao Madiwani wa Ufana Bernad Bajuta na wa Qameyu Bernad Fissoo, wamesema dunia ya sasa inahitaji kuwa na Mtandao wenye nguvu hivyo serikali iharakishe huduma hiyo muhimu.
Post A Comment: