Mkandarasi wa ujenzi wa Shule Shikizi ya Msingi ya Ponde iliyopo Kijiji cha Ponde Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Japhet Mikakalo |kulia}, akiwaongoza viongozi wengine kukagua ujenzi wa shule hiyo jana   jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Ramadhan Abdu fundi Mjenzi wa shule hiyo  , Mtunza stoo wa vifaa vya ujenzi wa shule hiyo , Mwalimu Allan Shemboza na  Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ponde, Omari Mbitemomo.

......................................................................


Na Dotto Mwaibale, Temeke

SHILINGI Milioni 800 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kujenga Shule Shikizi ya Msingi ya Ponde iliyopo Kijiji cha Ponde Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam zinakwenda kuwakomboa wanafunzi wa kijiji hicho ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kwenda maeneo mengine kusoma.

Wanafunzi hao walikuwa wakitembea zaidi ya kilometa tatu kila siku kwenda Kijiji cha Mikwambe na Mkokozi jambo ambalo lilikuwa likiwapa adha kubwa ya kutembea umbali huo kwa kwenda na kurudi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana  akiwa na  viongozi wa kijiji hicho na mkandarasi anayejenga shule hiyo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Toangoma, Wande Mkonyi alianza kwa kutoa shukurani nyingi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kutekeleza mradi huo mkubwa wa ujenzi wa shule hiyo ya Ponde.

Alisema shule hiyo ya Ponde itakuwa shule kubwa yenye  madarasa 22 kati ya hayo mawili yatakuwa kwa ajili ya elimu ya shule ya Chekechea ambayo itakuwa na bembea na vifaa vya michezo, kutakuwa na jengo la utawala, kichomea taka, maktaba, nyumba ya walimu ambayowataishi walimu wawili ‘Two in One’ na vyoo.

Alisema ujenzi wa shule hiyo unatokana na wingi wa wanafunzi katika shule tatu ikiwemo Shule Mama ya Toangoma ambayo inawanafunzi 3761, Shule ya Msingi Mikwambe ambayo ina watoto 3200 na Shule ya Msingi Mkokozi yenye wanafunzi zaidi ya 2900 hali ambayo inaonesha jinsi watoto walivyokuwa wakisoma katika mazingira magumu ya mrundikano hivyo kukamilika ujenzi wa shule hiyo itakuwa mkombozi mkubwa sana kwao.

Mkonyi alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Mkuu wa Wilaya  Mbunge, Diwani na viongozi wote wa Kijiji cha Ponde akiwepo Mkandarasi anayejenga shule hiyo Japhet Mikakalo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo na kamati ya ujenzi  kwa ushirikiano mkubwa ambao umeufanya ujenzi wa shule hiyo kuwa wa kasi na viwango vya hali ya juu.

Mkandarasi wa mradi huo Japhet Mikakalo alisema licha ya kuwepo kwa changamoto za hapa na pale lakini kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo kwa viongozi wote waliotajwa hapo juu pamoja na wananchi umefanikisha hatua hiyo ya kazi yenye ufanisi wa hali ya juu.

'' Binafsi nimshukuru sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na Afisa Elimu Msingi kwa kutupa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huu ambao unakwenda kuwakomboa watoto wetu kwani miradi ya namna hii kwa kuaminiwa na Serikali nimekuwa nikiitekeleza kwa viwango kulingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa,'' alisema Mikakalo.  

Mikakalo alisema mwaka wa fedha2022/ 2023 ulipokuwa umeisha kulikuwa na changamoto ya mfumo wa kifedha na kusababisha shughuli nyingi kukwama kwa kusubiri malipo lakini wao waliendelea kufanya kazi kutokana  vyanzo vingine ili kwenda na kasi ya kukamilisha mradi huo kwa wakati kwa ajili kuwasaidia wanafunzi hao kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi Toangoma, David Kulinga ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule hiyo ya Ponde alisema ujenzi wa shule hiyo ulianza Juni 27, 2023 na unatarajia kukamilika mwezi ujao na kuwa unakwenda vizuri na wana amini utakuwa tayari ndani ya wakati kutokana na kuwa katika hatua nzuri ya upauaji .

'' Matumaini ya kukamilisha kazi hii kwa muda uliopangwa yanatokana na kazi kubwa anayoifanya mkandarasi wetu Mikakalo ambaye wakati wote yupo eneo la ujenzi kuhakikisha kazi zinafanyika jambo ambalo linatutia moyo sana,'' alisema Kulinga.

Kulinga naye alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya si kwa Kata ya Toangoma bali kwa nchi nzima ya kujenga miundombinu ya shule.

Alisema wakiwa kama watendaji waliopo chini wana kila sababu ya kuunga mkono jitihada hizo za Serikali kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ambayo ni mkombozi katika kupata elimu watoto  na inakamilika kwa thamani ya fedha iliyokusudiwa na si vinginevyo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ponde, Omari Mbitemomo alisema mtaa huo ni kati ya mitaa 14 ambayo inaunda Kata ya Toangoma hivyo kupatikana kwa shule hiyo kuna kwenda kuwakomboa watoto wa eneo hilo ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kutunza miundombinu ya shule hiyo ikiwa ni moja ya njia ya kumheshimisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha za ujenzi wa shule hiyo.

Alisema watoto wa eneo hilo walikuwa na changamoto kubwa ya kwenda kusoma  mitaa ya Mwampembe eneo la Kizuda na Mikwambe ambapo walikuwa wakitembea umbali wa kilometa zaidi ya tatu na wengine walikuwa wakienda Shule ya Msingi, Mkokozi ambapo walikuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilometa zaidi ya mbili na nusu.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Toangoma, Wande Mkonyi, akionesha tabasabu kufuatia kazi nzuri ya ujenzi wa shule hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi Toangoma, David Kulinga akizungumzia ujenzi wa shule hiyo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ponde, Omari Mbitemomo. akizungumzia kuhusu maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo.
Mtunza stoo ya vifaa vya ujenzi wa shule hiyo, Mwalimu Allan Shemboza, akizungumzia umuhimu wa shule hiyo katika Mtaa huo wa Ponde..
Muonekano wa baadhi ya majengo ya shule hiyo ambao ujenzi wake unaendelea.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya shule hiyo.
Fundi akiendelea na kazi.
Ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo ukiendelea.
Fundi ujenzi wa shule hiyo, Ramadhan Abdu akizungumzia fursa ya kazi aliyoipata kupitia ujenzi wa mradi huo.
Mkandarasi wa ujenzi wa Shule Shikizi ya Ponde iliyopo Kijiji cha Ponde Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Japhet Mikakalo, akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ponde, Omari Mbitemomo.na Mtunza stoo ya vifaa vya ujenzi wa shule hiyo, Mwalimu Allan Shemboza.
Mafundi wakiendelea na kazi
Mkandarasi wa ujenzi wa Shule Shikizi ya Ponde iliyopo Kijiji cha Ponde Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Japhet Mikakalo akiwa mbele ya jengo la utawala wa shule hiyo ambayo ujenzi wake unaendelea.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: