Serikali yapongeza juhudi zinazooneshwa na sekta binafsi katika kuongeza ufanisi kwenye ubanguaji wa korosho nchini ili kufikia azma kuu ya kuacha kusafirisha korosho ghafi kwa mwaka 2026/27.

Hayo yamesemwa leo tarehe 21 Agosti, 2023 Wilayani Mkuranga na Naibu Waziri wa Kilimo, Mh. Anthony Mavunde alipotembelea kiwanda cha TANCOM kinachojihusisha na ukamuaji mafuta kutoka kwenye maganda ya korosho(CNSL)na kiwanda cha SABAYI INVESTMENTS cha kubangua korosho.

"Maelekezo na dhamira ya Mh. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuona ukuaji wa sekta ya kilimo unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, na ndiyo maana ameongeza bajeti ya kilimo kufikia bilioni 970 mwaka huu wa fedha yaani 2023/2024.

Moja ya eneo kubwa tulilolipa kipaumbele kama Serikali kupitia Ajenda 10/30 ni uongezaji wa thamani ya mazao ili kuondokana na kuuza yakiwa ghafi. Kwa upande wa korosho, tayari ekari 1,575.5 katika Kijiji cha Maranje Wilayani Nanyamba-Mtwara zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kongani kubwa ya viwanda ambavyo vitakuwa na uwezo wa kubangua tani 300,000 kwa mwaka.

Mkakati huu wa kubangua korosho zote zinazozalishwa nchini ifikapo mwaka 2026/2027 si tu utaongeza kipato kwa wakulima na halmashauri zetu, bali utaongeza fedha za kigeni na ajira kwa wananchi wa Taifa letu.

Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha mkakati huo wa kubangua korosho zote nchini unafikiwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji katika uongezaji thamani ya mazao ya kilimo na kutatua changamoto za kimsingi za wabanguaji korosho.

Nawapongeza viwanda vya TANCOM na SABAYI INVESTMENTS kwa uwekezaji huu mkubwa wa lengo la kuiongezea thamani korosho yetu.Serikali itakuwa naji bega kwa bega kuhakikisha lengo kuu la kuuza korosho iliyobanguliwa linafikiwa.”Alisema Mavunde

Akitoa taarifa kuhusu uwekezaji wa kiwanda cha kukamua mafuta kutoka kwenye maganda ya korosho cha TANCOM Bw. Erick Mkanda Meneja Uendeshaji alieleza kuwa Kiwanda hicho kinachomilikiwa na wawekezaji kutoka nchini Korea kina uwezo wa kuchakata tani 8000 za maganda kwa mwaka na ujenzi wa kiwanda kingine cha kubangua korosho tani 6000 kwa mwaka unaendelea. 

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Sabayi Investment Ltd., Bw. Daniel Marwa alieleza kwamba mwaka 2019 uwezo wa kiwanda ulikuwa ni kubangua tani 1000 ambapo baada ya kufunga mitambo ya kisasa, kwa sasa wana uwezo wa kubangua tani 10,000 za korosho kwa mwaka, na wameweka lengo la kufikia uwezo wa kubangua tani 40,000 miaka mitatu ijayo ili kuunga mkono jitihada za Mh Rais katika uongezaji wa thamani wa korosho.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mheshimiwa Khadija Nassir aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka mkazo katika uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza Wilayani Mkuranga kwani fursa ni kubwa.









Share To:

Post A Comment: