Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu bora ya elimu katika Mkoa wa Dodoma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Shule mpya za Msingi na Sekondari, ujenzi wa maabara na mabweni katika Wilaya zote zilizopo Mkoani Dodoma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule kwa nyakati tofauti wilayani Chemba katika ziara yake ya kikazi ya kukagua hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya elimu wilayani humo.
“Ninatembelea Wilaya zenye changamoto ambazo bado hazijakamilisha miradi yake kama ilivyopangwa. Hapa Magugu ujenzi wa hii shule ulitakiwa kukamilika Juni 30, 2023 na leo ni tarehe 3 Agosti, wako katika hatua za ukamilishaji, hata hivyo ujenzi wa choo bado haujakamilika,kazi hizi zilikuwa ziende Pamoja” Senyamule alihoji.
Aidha, ametoa muda wa siku saba kwa Mkuu wa Shule hiyo kukamilisha ujenzi wa choo ili shule hiyo iweze kuanza kutumika.
“Tunategemea maelekezo na ushauri vifanyike kwa wakati mmoja,nimeshaelekeza ununuzi wa vifaa vyote ufanyike kwa pamoja kusiwe na ucheleweshaji wa aina yoyote ile na sababu zisizo na msingi.
Katika hatua nyingine Mhe. Senyamule amemwagiza Mwl Mkuu wa Shule hiyo ya Magungu Mwl. Edwin Fredrick kuthaminisha nguvu kazi inayochangiwa na wananchi.
“Thaminisheni mchango wa wananchi, wapewe taarifa kuwa mchango wao wa nguvu kazi ni shilingi ngapi, ili fedha inayobaki kutokana na mchango wa nguvu za wananchi ziweze kufanya kazi nyingine mfano Ujenzi wa nyumba za walimu.
Pia, ameagiza kukamilishwa kwa ujenzi wa vyoo katika shule hiyo ndani ya wiki moja, huku akiwataka kuongeza kasi katika miradi inayoendelea ya Sequip na Madarasa ya kidato cha Tano.
“Hatuwezi kuwa na mpango wetu kama Mkoa wa kukamilisha miradi ya ujenzi na wewe mwalimu una mpango wako, hii ni kazi ya Serikali, nitarudi ndani ya wiki moja” Senyamule amesisitiza
Mkoa wa Dodoma kupitia mradi wa Boost umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10.6 kwa ajili ujenzi wa Shule mpya 16, vyumba vya madasa ya msingi 163, madarasa ya awali 16, ujenzi wa vyoo 106, nyumba za walimu 03 na darasa 01 la elimu maalumu. Wilaya ya Chemba imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 na Kondoa Mji na Halmashauri Shilingi Bilioni 1.7.
Katika ziara hiyo Mhe. Semnyamule alipata fursa ya kukagua Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Babayu,Shule mpya ya Msingi Magungu, Ujenzi wa mabweni na madarasa katika shule ya Sekondari Msakwalo pamoja na kufanya Mkutano wa kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi katika kata ya kwa mtoro Kijiji cha kwa mtoro.
Post A Comment: