Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka ametoa wito kwa Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kutangaza fursa za Biashara ya Kaboni ili wananchi wapate mwako wa kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti hivyo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Mtaka ametoa rai hiyo Agosti 4, 2023 wakati alipotembelea Banda la Ofisi hiyo ya katika Maonesho ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
Ameshauri kutumia vyombo vya habari kuzungumzia manufaa na faida za biashara ya kaboni hususan msisitizo wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango kuhusu faida ya biashara hiyo.
Pia, Mhe. Mtaka ameshauri iandaliwe programu maalum ya vipindi vya elimu kwa umma vinavyoelimisha wananchi kuhusu fursa, manufaa na mafanikio yaliyopo katika masuala ya Muungano na hifadhi endelevu ya Mazingira.
Ameongeza kuwa vipindi vinavyozungumzia ya Muungano na Mazingira vina mchango mkubwa katika kuelimisha umma kwani na vitawawezesha Watanzania wengi kufahamu msingi na historia ya Muungano pamoja na majukumu mengine muhimu yanayotekelezwa na Ofisi hiyo.
Hali kadhalika, Mkuu wa Mkoa huyo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ni kubwa hivyo majukumu mahsusi inayotekeleza yanapaswa kutambulika na umma, hivyo ni muhimukuyatangaza kwa kuandaa maudhui ya vipindi na makala mbalimbali zitakazotangazwa kupitia vyombo vya habari vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii.
Aidha Mtaka amesema uaandaji, utengenezaji na urushaji wa vipindi vya elimu kwa umma ni moja ya njia za haraka ya kutangaza shughuli na majukumu ya Wizara ili kuweza kutambulika na kufahamika kwa wadau na jamii na hivyo kuvitaka Vitengo vya Mawasiliano Serikalini kuachana na mfumo wa kutumia matukio katika kutoa habari na taarifa kwa umma.
“Yapo masuala muhimu ya kihistoria ya Tanzania ambayo bado jamii ya Watanzania ikiwemo historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hatua inayotokana na baadhi ya watu kutopenda kujifunza, hivyo ni wajibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais kuzalisha vipindi na machapisho mbalimbali yanayoeleza chimbuko, misingi na historia hiyo,“ amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Kuhusu elimu ya uhifadhi wa mazingira, Mtaka ameitaka Ofisi hiyo pia kuandaa makala na vipindi vya televisheni na redio zinazofafanua kwa undani dhana na tafsiri halisi ya biashara ya kaboni kwani biashara hiyo kwa sasa ni fursa na mkombozi wa kiuchumi kwa jamii zilizopo katika ukanda wa maeneo ya misitu nchini.
Kwa upande wake Afisa Mazingira Mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Lungo amemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa maoni na ushauri aliotoa kwa Ofisi hiyo kwa kuwa yatasaidia kuongeza kasi, ubunifu na ufanisi katika kujitangaza zaidi na kuhakikisha kuwa majukumu ya ofisi hiyo yanafahamika kwa wadau na umma kwa ujumla.
Post A Comment: