..................................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
ABIRIA wenye uzalendo na nchi wanaosafiri kwenye mabasi ndani na nje ya nchi wamemuomba Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuiruhusu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kutoa motisha kwa wananchi wanaotoa taarifa za mabasi yanayokwepa kukata tiketi za mtandao kwa lengo la kuikosesha Serikali kupata mapato.
Motisha wanayoiomba abiria hao ni ile inayotokana na LATRA baada ya kuyatoza faini mabasi
wanayotoa taarifa za kukwepa kulipa kodi
kwa njia ya tiketi za kimtandao.
Ombi la abiria hao limekuja ikiwa zimepita siku chache tangu Kamati ya
Bunge ya Miundombinu kuipongeza LATRA kwa ufanisi wa kazi ambapo Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi hiyo, CP Habib Suluo, aliihakikishia kamati hiyo kuwa mamlaka
hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuboresha shughuli za
usafirishaji nchini.
Suluo alitoa ahadi hiyo baada ya Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Miraji Mtaturu, kuipongeza LATRA
kwa kusimamia mfumo wa utoaji tiketi kwa njia ya mtandao ambao umeanza kupunguza kero
kwa abiria.
'' Tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa ukamilifu na kuufanyia kazi
ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa lengo la kuboresha
shughuli za usafirishaji ikiwemo kuendelea kuwatahini madereva ili kuhakikisha
abiria wanasafiri kwa usalama,''. alisema Suluo wakati akiwasilisha taarifa ya
mamlaka hiyo kwa wabunge wa kamati hiyo Agosti 25, 2023.
Mmoja wa abiria hao aliyekuwa amesafiri na basi la Kampuni ya Nyahunge
akitokea Dodoma kwenda Singida aliyetoa taarifa kwa Mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo na Afisa Mfawidhi wa
LATRA Mkoa wa Singida Layla Dafa baada ya kushuhudia abiria wakikatiwa tiketi
zisizo za kielektroniki zilizopigwa marufuku kwa lengo la kuinyima Serikali mapato alisikitishwa na kitendo cha Afisa Habari wa
Mamlaka hiyo Salum Pazzy kushindwa kuwasiliana na abiria huyo licha ya CP Suluo
kumpa namba ya Mhasibu Mkuu wa LATRA, Samwel Kaenja ili amuunganishe abiria
huyo na Afisa Habari huyo kufuatia mabasi manne ya kampuni hiyo kupigwa faini
ya Sh. Milioni 1,250,000/- likiwepo basi moja la Kampuni ya Supafeo.
'' Nimempa namba yako Afisa Habari wetu Mkuu Salum Pazzy kama ulivyoagizwa
na mkurugenzi atakupigia sasa hivi,'' alisema Kaenja..
Abiria huyo alisema pamoja na kumpigia simu mara kadhaa na kwa siku tofauti
na kumtumia 'link' kwenye namba yake ya WhatSapp zinazoonesha taarifa hiyo
ilivyoandikwa kwenye mitandao ya kijamii simu ya afisa habari huyo ilikuwa ikiita wakati wote
bila ya kupokelewa jambo ambalo linaonesha haendi na kasi ya utendaji wa kazi
wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbawar na Mkurugenzi wake CP Suluo na kuomba
ikiwezekana aondolewa kwenye nafasi hiyo na kuwekwa mtu mwingine kwani
anafifisha utendaji kazi wa mamlaka hiyo licha ya mkuu wake kutoa ahadi kwa
Bunge ya kuboresha ufanisi wa kazi.
Alisema utendaji kazi wa aina ya Afisa Habari huyo unaweza kuwakatisha
tamaa wananchi ya kutoa taarifa za namna hiyo jambo ambalo litaisababishia
Serikali kukosa mapato yanayosaidia kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kulipa mishahara ya watumishi akiwemo na afisa huyo.
'' Kitengo cha habari na masoko ndio kiunganishi kati ya wananchi na mamlaka
hiyo sasa inapofikia hatua ya wahusika kupigiwa simu kwa zaidi ya siku mbili na
kwa nyakati tofauti lakini hakuna mapokeo yoyote kinakuwa hakina maana ya
kuwepo na hiyo inaonesha kutokuwepo kwa umakini na kufanya kazi kimazoea,''
alisema abiria huyo kwa niaba ya wenzake.
Aidha abiria hao wamempongeza Mkurugenzi Mkuu wa LATRA kwa kazi nzuri
anayoifanya ndani ya mamlaka hiyo pamoja na Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa
Singida, Layla Dafa kwa hatua aliyoichukua ya kutuma Afisa wake Kilua Mbezi
kuyafutilia mabasi hayo Stendi Kuu ya
Mabasi Mkoa wa Singida Misuna na kubaini kosa hilo na kuyatoza faini ambapo
alitumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa abiria kuhusu umuhimu na faida ya kupatiwa
tiketi za mtandao na kuwa kabla ya kupanda gari nilazima wapatiwe tiketi hizo
na kama watapewa za zamani ambazo zimepigwa marufuku watoe taarifa kwa kupiga
namba ya bure 0800110020.
Aidha, Mbezi aliwakumbusha wafanyakazi wa mabasi hayo kuendelea kufuata sheria za usafirishaji ili kuepuka adhabu mara watakapobainika kutenda makosa na kuwa jambo hilo lipo ndani ya uwezo wao na kuwa wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuwabaini wanaokiuka sheria na kutoa elimu hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habib Suluo, akisaini kitabu wakati akiwa katika moja ya matukio yake ya kikazi
Post A Comment: