Na,Jusline Marco;Arusha


Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema kuwa ofisi ya Mkoa wa Arusha itahakikisha inawaunga mkono wadau wa mnyororo wa thamani wa kilimo ili kuhakikisha dhamira njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu katika kuinua kilimo inafikia malengo.

Akimwakilisha Mkuu huyo wa Mkoa katika utoaji wa zana za kilimo kwa wakulima katika maonesho ya nanenane Kanda ya Kaskazini Afisa Kilimo Mkoa wa Arusha Bwn.Daniel Loiruki amesema dira ya 2030 imelenga kuhakikisha kilimo kinakua kwa asilimia 10 ambapo katika ukuaji huo wadau wa sekta binafsi ,taasisi za kifedha wanahitajika ili kuweza kufikia azma hiyo.

Aidha ameipongeza kampuni ya PASS TRUST kupitia kampuni tanzu ya PASS Leasing kwa kuhakikisha wanamfikia mkulima ambaye ni mlengwa katika zoezi zima la uzalishaji, ambapo pia katika kutekeleza hayo wameshirikiana na wadau wengine ikiwemo kampuni ya Agricom Afrika.

"Katika urahisi huo zana zenyewe zinakuwa ni zana ambazo zinatumika kama dhamana na mkulima ahitaji kupeleka kiwanja kama dhamana kwa hiyo mkulima anaurahisi mkubwa wa kuhakikisha kwamba anapata zana hizi."alisema Loiruki

Ameongeza kwa kuwataka wakulima kutambua kuwa tija katika kilimo ni pamoja na maandalizi mazuri ya eneo la shamba pamoja na zana bora zinazopatikana kwa bei nzuri huku akisisitiza kuwa, kupitia zana hizo mkulima atapata faida ambapo amewataka wakulima kulima mazao huku wakijua masoko yao yanapatikana wapi na ni bidhaa gani zinahitajika sokoni zikiwa na ubora unaohitajika.

Kwa upande wake Meneja wa PASS TRUST Kanda ya Kaskazini Bi.Hellen Wakuganda amesema kuwa Kampuni hiyo ya kidhamini ambayo inamuangalia mdau wa kilimo pale ambapo anakuwa na changamoto za kimtaji na kuchukuwa jukumu la kuandaa andiko ili taasisi ya fedha iweze kumuelewa mkulima na kumpatia mkopo.

Ameeleza kuwa baada ya kuandika andiko hilo Kampuni ya PASS inaingia katika jukumu la pili la kumdhamini mkulima kwa kumuongezea dhamana ili kuhakikisha mkulima anapata bidhaa aliyoihitaji kulingana na kilimo anachoenda kukifanya.

Naye Meneja Biashara kutoka kampuni tanzu ya PASS Leasing Tanzania inayomilikiwa na kampuni mama ya PASS TRUST , Bi.Maria Wambura katika hafla hiyo ya utoaji wa zana za kilimo amesema kuwa kama Pass leasing huanzia shambani katika maandalizi ya shamba, uvunaji,usafirishaji pamoja na uchakataji wa mazao.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya kampuni hiyo wameweza kuwafikia wakulima wanufaika zaidi ya 700 kwa zana zenye thamani ya shilingi bilioni 35 ambapo kati ya hao asilimia 20 ya wanufaika ni vijana huku asilimia 10 wakiwa ni wanawake ambapo amesema kama Pass leasing katika mkakati wake wa mwaka 2026 wanategemea kuwafikia akina mama kwa asilimia 50 ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano.

Pamoja na hayo amesema kuwa kampuni ya Pass leasing inafanya kazi na wabia mbalimbali wa zana za kilimo pamoja na makampuni ya bima ambapo jumla ya trekta 4 ikiwemo Power tiler na Kubota kutoka kampuni ya Agricom na Zana bora pamoja na mashine moja ya kukamua alizeti zimeweza kukabidhiwa kwa wakulima katika maonesho ya nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Themi Njiro Jijini Arusha.

Ameongeza kuwa zana hizo zilizokabidhiwa kwa wakulima hao zimekatiwa bima ambayo itaweza kusaidia wakati wa majanga yatakapotokea ambapo kati ya wakulima wanaobidhiwa zana hizo miongoni mwao yupo kijana na hiyo ni kuonyesha kuwa wanaiishi kauli mbiu ya nanenane ya mwaka huu ya "Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula."

Katika hatua nyingine Meneja wa Kanda ya Kati na Kaskazini kutoka katika Kampuni ya Agricom Afrika,Peter Temu amesema kuwa wamekuwa wakifanya kazi kwa ukaribu na taasisi za kifedha ambazo zinawawezesha wakulima, ikiwemo kampuni ya Pass Trust ambapo kwa kipitia njia hiyo wameweza kuwasaidia wakulima wengi kuweza kufanikisha malengo yao ya kuweza kupata zana zilizo bora katika kufanya kilimo.

Share To:

Post A Comment: