NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Maji Mhe.Maryprisca Mahundi amefanya ziara kutembelea Mradi wa Usambazaji wa Majisafi kati ya Makongo na Mji wa Bagamoyo ambapo amewapongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kwa jitihada ambazo wanazifanya katika maeneo ambayo yamenufaika na mradi huo.

Akizungumza kwenye ziara hiyo leo Agosti 19,2023 mpaka sasa kwa kiwango kikubwa wananchi wameweza kupata maji kwa uhakika katika maeneo mengi ambayo mradi huo umepita na wataendelea kuwafikia wale wote ambao hawajafikiwa na huduma ya majisafi na salama ili wananchi waweze kuwa na uhakika na upatikanaji wa maji kwenye maeneo yao.

Aidha Naibu Waziri amesema Wizara inaendelea kusambaza mita ambazo utakuwa unalipia kabla ya matumizi ili kuondokana na ulimbikizaji wa bili.

Amesema wasomaji wa mita wa DAWASA wanatakiwa kushika taratibu ambazo wamejiwekea kuondokana na malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wateja wao.

Pamoja na hayo amewapongeza DAWASA kwa kuendelea kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Kinondoni katika kuhakikisha wanashughulikia kero ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara kwa wananchi hususan kwenye masuala ya maji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Mhandisi Shabani Mkwanywe ambaye amemuwakilisha Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA kwenye ziara hiyo, amesema maeneo kuanzia Makongo mpaka Bagamoyo asilimia 80 hadi 90 ya wananchi wamepata huduma ya majisafi na bado kuna sehemu chache ambazo hawajakamilisha na wanaendelea na jitihada za kukamilisha hususan yale maeneo ambayo yalikuwa nje ya mradi.

"Tupo tayari wakati wowote kushirikiana na wadau katika kuhakikisha kwamba huduma ya maji inakuwa bora zaidi na ingawa bado kuna changamoto chache ambazo tunaamini ndani ya mwaka huu wa fedha tunaenda kuzimaliza na wananchi wapate maji kwa uhakika". Amesema

Nae Mwakilishi wa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Goba, Bw. Emirick Msuya amesema kwasasa upatikanaji wa majisafi ni mzuri ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo maji yalikuwa yanapatikana kwa shida na ukizingatia katika zahanati hiyo uhitaji wa maji ni mkubwa.

Kwa upande wa wananchi wa Mivumoni Wazo Jijini Dar es Salaam, wameipongeza Serikali kwa kuwaondolea kero ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo, ambapo kwa sasa maji yanapatikana kwa uhakika.









Share To:

Post A Comment: