Na Moreen Rojas,Dodoma.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) inakusanya mapato ya takriban Shilingi bilioni mbili kila mwezi kutoka kwa wananchi wanaotoa fedha zao kulipia huduma mbalimbali hospitalini hapo.


Akizungumza leo katika Ukumbi wa Idara ya Huduma za Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amesema mapato  hayo  yameongezeka kutoka shilingi milioni 900 kwa mwezi.


Aidha, Prof. Janabi ameeleza kuwa fedha hizo zimeusaidia uongozi wa hospitali hiyo kutumia Shilingi bilioni 14 kuwalipa posho na marupurupu wafanyakazi wake.


Pia, Prof. Janabi amearifu kwamba hospitalini hapo huwasili wagonjwa 6,200 kila siku kwa ajili ya kufuata matibabu huku wanafunzi 2,000 kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wakiwasili kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo.


"Kusukwa Upya Huduma za Wagonjwa wa Nje (OPD) na Wagonjwa Waliolazwa (IPD)Kwa nyakati tofauti, Serikali kupitia Wizara ya Afya ikitoa maelekezo ya kuhakikisha sisi watoa huduma tunatoa huduma bora. Napenda kutoa taarifa kuwa maelekezo haya tumeyafanyia kazi kwa kina na tunaendelea kuyafanyia kazi kila siku. Hospitali ina OPD ambayo inaona takribai wagonjwa 900 hadi 1,000 kwa siku hivyo tumeiboresha"Amesema Prof.Janabi



Vilevile, mtaalamu huyo amebainisha kwamba hospitali hiyo hutoa huduma kwa muda wa masaa 24 kwa siku ili kumsaidia mwananchi kupata huduma za afya muda wote.


Aidha ameongeza kuwa hospitali ya Taifa Muhimbili ilifanya tathimini na kubaini kuwa kwa siku moja eneo hilo wanaingia watu 20,000 na magari 3,500. Hali hii imekuwa changamoto kwani ndugu wa wagonjwa na wafanyakazi walikua wakikosa mahali pa kuegesha magari yao. Tathimini hiyo ilionesha kuwa kuna baadhi ya watu wanaegesha magari yao ndani kutokana na usalama uliopo, kutokuwepo mfumo wa malipo ya maegesho ambapo wakishaegesha huenda kufanya shughuli zao Kariakoo au mjini.


"Hali hii ilitulazimu kuanzisha utaratibu wa kulipia huduma ya maegesho ili isaidie kupunguza msongamano wa magari ndani ya Hospitali. Jitihada za kupunguza msongomano Upanga ziligusa pia kuhamisha huduma tatu kwenda Mloganzila kwa lengo lile lile la kupunguza msongamano mkubwa uliokuwepo MNH Upanga. Hali kadhalika tulipunguza idadi ya ndugu wanaokuja kusalimia wagonjwa waliolazwa kutoka watano kwa wakati mmoja hadi wawili asubuhi, mmoja mchana na wawili jioni. Utaratibu huu unalinda watumiaji wa huduma wakiwemo wagonjwa na wageni wote wanaongia wanaoingia na kutoka ndani ya Hospitali"Amesisitiza Prof.Janabi



Katika Kipindi cha mwaka 2022&2023, Hospitali ilipokea fedha za UVIKO-19 TZS. 11,876,800,000 Bil. kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kama MRI, CT-Scan, Mtambo wa tiba radiolojia (Interventional radiology equipment), vifaa vya ICU, ujenzi na ukarabati wa idara ya magonjwa ya dharura na kitengo cha dharura kwa kina mama wajawazito. Vifaa hivyo vilinunuliwa na kusimikwa kama ilivyopangwa. Na kwa sasa vimeanza kutumika.



Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: