Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akijibu maswali ya Wajumbe wa Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI wakati kamati hiyo ilipokuwa ikipokea taarifa ya usambazaji wa bidhaa za Afya kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai katika kikao cha Kamati kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma. jana.
.....................................................
Na WAF, Dodoma
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya
UKIMWI imeitaka Bohari ya Dawa (MSD) nchini kuongeza kasi ya usambazaji wa
bidhaa za Dawa pamoja na kuwa na maghala ya dawa katika kila Halmashauri.
Wito huo umetolewa leo Mwenyekiti wa kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI, Mhe. Stanslaus Nyongo baada ya
kupokea taarifa ya usambazaji wa bidhaa za Afya kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa
Bohari ya Dawa (MSD) Bw. Mavere Tukai katika kikao cha Kamati kilichofanyika
Bungeni Jijini Dodoma.
“Kwanza naipongeza sana Wizara kwa hatua
mnazoendelea kuchukua za kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za Dawa na vifaa
tiba inaongezeka lakini pia niwatake muongeze jitihada hizo kwakuwa uhitaji wa
bidhaa hizo ni mkubwa nchini”, ameeleza Mhe. Nyongo
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu
wakati akijibu maswali ya Wajumbe wa kamati hiyo amesema Serikali imewapa mtaji
Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kuhakikisha Dawa na vifaa tiba zinapatikana kwa
wakati na kusambazwa nchini.
“Tumepokea mapendekezo yote ya kamati, Serikali
tutahakikisha tunaiwezesha MSD ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo pamoja na
kuwafutia madeni waliyonayo”, amesema Waziri Ummy
Pia, Waziri Ummy ameitaka MSD kujipima katika
upatikanaji wa Dawa, Vifaa tiba pamoja na vitendanishi kwenye huduma za Afya
ngazi ya msingi.
Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bw.
Mavere Tukai wakati akiwasilisha taarifa yake kwa kamati hiyo amesema
usambazaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kupitia
Mfumo wa Ugavi Shirikishi umefanikiwa kwa asilimia 97.
Pia, amesema kwa Mwaka wa fedha 2022/23, Bohari
ya Dawa ilianza usambazaji wa bidhaa za afya mara Sita kwa mwaka badala ya mara
Nne kama ilivyokuwa awali.
“Lengo la usambazaji huu ni kupunguzia vituo vya kutolea huduma za afya muda wa kusubiri bidhaa hivyo kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za Afya nchini”, ameeleza Bw. Mavere.
Post A Comment: