.........................................................
Na Mwandishi wetu- Dodoma
BOHARI ya Dawa (MSD) imewahakikishia wananchi
huduma bora zinazokidhi viwango vya Kimataifa kutokana na hatua
zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha utendaji wake.
Akieleza hatua hizo Agosti 24, 2023 jijini Dodoma wakati wa
mahojiano maalum na Idara ya Habari (MAELEZO), Mkurugenzi Mkuu wa Bohari hiyo
Bw. Mavere Tukai amesema, MSD inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhi bidhaa za afya katika
mikoa mitano ikiwemo Dodoma na Mtwara ambapo mkandarasi ameanza
kazi ya ujenzi.
“Mradi huu hapa jijini Dodoma na kule mkoani
Mtwara inagharimu shilingi Bilioni 39 ikiwa ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa
maghala matano tuliyopanga kujenga katika Ofisi za Kanda katika mikoa ya
Mwanza, Kagera na Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha huduma zetu kwa
kuzisogeza zaidi kwa wananchi, kupanua uwezo wa miundombinu yetu hali
itakayopunguza umbali wa kufuata bidhaa za afya Dar es Salaam”, amesisitiza Bw.
Tukai.
Akieleza zaidi, Bw.Tukai amesema, maghala hayo yatakapokamilika
yatakuwa na uwezo wa kutoa huduma kama ilivyo ghala la Dar es Salaam, hivyo
uwekezaji huu utakuwa na faida nyingi ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji,
kusogeza zaidi huduma kwa wananchi, kupunguza muda wa kufikisha bidhaa za afya
kwa watoa huduma, kuwepo kwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA na kuongeza uwezo wa
kuhifadhi bidhaa za afya kwa kuzingatia viwango vya kimatifa.
Sanjari na faida za uwekezaji huo, Bw. Tukai
ameongeza kuwa, MSD imejipanga kujiendesha kibiashara hivyo kutimiza azma ya
kunzishwa kwake kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuzalisha faida
itakayosaidia kuimarisha zaidi huduma zake kwa wananchi.
“Hatua hizi zitaenda sambamba na kujiimarisha
katika utoaji wa huduma Kimataifa hasa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo tuna jukumu la kuzihudumia”,
alisisitiza Bw. Tukai.
Aidha, Bw. Tukai amesema kuwa MSD imechukua hatua
za kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija.
Ujenzi wa Maghala yote matano utakapokamilika
unakadiriwa kugharimu Serikali kati ya
Shilingi Bilioni 90 hadi 95 za Kitanzania hali itakayoiwezesha MSD kuimarisha
zaidi utendaji wake kwa kutumia mifumo
ya kisasa zaidi katika utoaji wa huduma zake..
Post A Comment: