Na.Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amekabidhi matofali 500 yenye thamani ya Sh 650,000 ili kusaidia ujenzi wa vyoo vya nje kwenye Zahanati ya Kijiji cha Samaka kilichopo Wilayani Ikungi Mkoani Singida.
Kukamilika kwa Zahanati hiyo itapunguza changamoto kwa akina mama na wananchi ya kutembea umbali mrefu kwenda Dung'unyi na Ikungi kufuata huduma ya afya.
Akikabidhi matofali hayo Julai 31,2023, Katibu wa Mbunge wa Jimbo hilo Ally Rehani amesema huo ni muendelezo wa mbunge kuchangia ujenzi huo ikiwa ni jitihada zake za kuinga mkono serikali katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema Mtaturu ametoa matofali hayo ili kuhakikisha Zahanati hiyo inaanza kutoa huduma mapema.
"Tofali hizi nazitoa kwa niaba ya mbunge Mtaturu ambaye alitamani awepo hapa mwenyewe ili akabidhi,lakini kutokana na majukumu mengine ameshindwa kufika hapa,hivyo nipo hapa kwa niaba yake ili kukamilisha dhamira aliyonayo ya kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto zao," amesema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Dung'unyi Mathias Casmiry akipokea matofali hayo amemshukuri sana Mbunge Mtaturu kwa moyo wake wa upendo na wa kujitolea kila mara.
"Ndugu zangu Zahanati hii hadi inafika hapa Mtaturu amekuwa chachu kubwa sana na bado hajachoka kutuunga mkono,nifkishie salamu zangu kwake kuwa tunamshukuru sana,"amesema Diwani huyo.
Aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea fedha nyingi za maendeleo katika miradi ya Elimu,Umeme,Barabara,Maji na Afya kwenye kijiji cha Samaka.
Mbunge Mtaturu kwa kushirikiana na wananchi na wadau walianza kujenga Zahanati hiyo Mei 2022,ambapo Mbunge Mtaturu alitoa vifaa mbalimbali ikiwemo matofali,saruji na nondo vyenye thamani ya Sh Milioni 7.8 na baadae serikali kupeleka Sh Milioni 50 ili kumalizia ujenzi huo.
Post A Comment: