Na John Walter-Manyara

Zaidi ya Wafanyabiashara 800 kutoka Manyara na mikoa mbali ya Tanzania na nje ya mipaka ya nchi  wanatarajiwa kushiriki maonesho ya pili ya biashara ya Kimataifa mkoani Manyara (TANZANITE MANYARA TRADE FAIR ) yanayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji mkoani hapa.

Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema maonesho hayo yatafungua fursa mbalimbali za kibiashara kwa kuwa yatawakutanisha wadau mbalimbali wa ndani na hata nje ya nchi.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara kushiriki katika maonesho hayo ya pili yatakayofanyika katika uwanja wa Stendi ya zamani kuanzia Oktoba 17-21,2023, kuchangamkia fursa zilizopo na kuongeza kuwa hiyo ni nafasi nzuri kwa wajasiriamali kukuza na kujenga mtandao wa kuinua biashara.

Amesisitiza wajasiriamali watakaoshiriki, kuweka vifungashio vitakavyoutangaza mkoa wa Manyara.

Aidha amesema wanafanya mazungumzo na hifadhi za taifa zilizopo mkoani hapa kuongeza idadi ya wanyamapori katika maonesho hayo.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoa wa Manyara Mussa Msuya amesema Maonesho hayo yatawezesha wafanyabiashara kukutana na kutangaza bidhaa na huduma  zao pamoja na kutafuta masoko mapya.

Mdhamini mkuu wa Maonyesho hayo Kampuni ya Mati Super Brands Ltd chini ya mkurugenzi wake David Mulokozi ambaye pia ni Makamu mwenyekiti Viwanda (TCCIA) amesema maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee kwa kuwa Kampuni hiyo inayozalisha vinywaji viburudishi vinavyopendwa na wengi ndani na nje ya nchi, itakuwa na mambo mengi mazuri.

Kaulimbiu ya Maonyesho ya biashara ya TANZANITE TRADE FAIR mwaka 2023 ni Manyara na Fursa za kibiashara.


Share To:

Post A Comment: