Na. Majid Abdulkarim, Mbarali
Madaktari Bingwa wa macho wameweka kambi ya wiki moja Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kwa ajili ya kuwatafuta wagonjwa wenye matatizo ya mtoto wa jicho ambapo mpaka sasa wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho kwa siku ya leo.
Hayo yameelezwa na Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za macho kutoka Wizara ya Afya Dkt. Bernadetha Shilio wakati wa kliniki ya kuwatafuta wagonjwa hao wilayani humo ambapo amesema kambi hiyo imefadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Helen Keller.
Dkt. Bernadetha amesema kambi hiyo ilianza Agosti 14 mwaka huu na inatarajiwa kuendelea wiki nzima huku wakiifanya nyumba kwa nyumba ili kubaini wagonjwa wenye tatizo la matoto wa jicho na kuwafanyia upasuaji.
Amesema mpaka sasa wamewafikia wagonjwa 800 ambapo amesema wanatarajia kufanya upasuaji kwa macho 500 kwani kuna baadhi wanaweza kufanyiwa macho yote mawili.
Meneja huyo amesema mpaka sasa wamefanya upasuaji kwa wagonjwa 20 na wengine wanaendelea na uchunguzi ili huduma ya upasuaji iweze kuendelea kutokana na uchunguzi wa awali utakao kuwa umefanyika.
“Huduma hii ni ya kipekee kidogo kwa sababu wagonjwa hawa wanatafutwa kwenye nyumba zao wakipatikana wanafanyiwa uchunguzi wa awali halafu wanakuja kwenye kambi kabla ya kufanyiwa upasuaji,”amesema Dkt. Bernadetha.
Amesema madaktari wawili bingwa kutoka Hospitali ya Kanda ya Mbeya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya kwa pamoja wanashirikiana katika kufanya upasuaji na tayari walipata mafunzo ya ziada kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wengi katika kipindi kifupi lakini kwa matokeo mazuri zaidi.
Amesema wanashukuru tangu upasuaji huo umeanza zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanapata matokeo mazuri na wagonjwa wametoa ushuhuda wa hilo.
Vile vile ameeleza kuwa wanalenga kufika katika mkoa wa Njombe kwa ajili ya kuwafanyia upasuaji wagonjwa watakao bainika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho.
Ameweka wazi kuwa wanaopata ugonjwa wa mtoto wa jicho ni wazee na wanakosa watu wa kuwasindikiza kwa kuzingatia kwamba hawaoni kwahiyo huduma hiyo inawakomboa na kuwasaidia kushirikiana na jamii na inachangia katika maendeleo ya nchi.
Dkt. Bernadetha ameongeza kuwa mradi huo umeletwa katika Wilaya ya Mbarali kwa sababu kulikuwa na mradi mwingine wa vikope ambao unaenda nyumba kwa nyumba.
Lakini pia ameeleza kupitia mradi wa vikope baadhi ya waliofika walionekana wana tatizo la mtoto wa jicho ndio sababu ya kuupeleka mradi huo Wilayani humo.
“Hata hivyo Mbarali kulikuwa na uhitaji mkubwa kutokana na uhaba wa wataalamu wa macho kwa ujumla kwa ajili ya upasuaji pamoja na vifaa kupitia mradi huo tumeweza kupata vifaa na wataalamu,”amesisitiza Dkt. Bernadetha
Aidha amebainisha kuwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania inakadiriwa kuwa, asilimia moja ya watu wana ulemavu wa kutokuona kabisa huku asilimia 50 kati ya hiyo ni kwa sababu ya mtoto wa jicho.
“Lakini kuna wengine wana uwezo wa kuona kwa uwezo wa kati na ule wa juu na hii kama asilimia Tatu ya wananchi kwa ujumla na zaidi ya asilimia 70 inachangiwa na mtoto wa jicho hivyo tatizo hilo ni kubwa kwani kila mwenye miaka 40 yupo hatarini kupata mtoto wa jicho tunahimiza watu wafike Hospitali mapema na kupata tiba”, amesema Dkt. Bernadetha.
Mwisho, amesema kutokana na mabadiliko ya mtu kuwa mtu mzima mara nyingi nywele zinakuwa nyeupe na kwenye macho kuna lensi inabadilika, kinachofanyika katika kambi hiyo ni kuondoa lenzi yenye shida na kuweka lenzi ya kioo ili kumuwezesha mtu kuona vizuri, aidha katika upasuaji huo hauhusishi kuweka jicho la mnyama.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mratibu wa Macho kutoka Ofis ya Rais TAMISEMI Ernest Paul amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi Milioni 50 katika kila Halmashauri nchini ili kuboresha Huduma za macho katika ngazi ya msingi.
Bw. Paul ametoa wito kwa wakazi wa Wilaya ya Mbarali kujitokeza kwa wingi na kupatiwa Huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho ili kuepuka ulemavu wa kutokuona na jamii kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo.
Post A Comment: