MBUNGE wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi amemtaka Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilombero pamoja na Bodi ya Maji Mngeta kukutana na wananchi wa Kijiji cha Ikule Kata ya Mngeta ili kutoa elimu juu ya uendeshaji wa mradi wa maji kijijini hapo.


Kunambi ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kusikiliza changamoto za wananchi katika Kata ya Mngeta ambapo wananchi wa Kijiji hiko cha Ikule walilalamika kutozwa kiasi kikubwa cha fedha cha malipo ya maji.

" Haiwezekani nimepambana kupata fedha za kuleta mradi mkubwa maji hapa na Rais Samia Dkt Samia Suluhu Hassan akatupatia zaidi ya Sh Milioni 600 halafu bado wananchi wetu hapa walalamike kuteseka. Wananchi hawa hawapaswi kulalamikia kero kama hii wakati tayari ilishatatuliwa.

Niwatake RUWASA na Bodi ya Maji ndani ya siku saba mje hapa mtoe elimu kwa wananchi hawa na kumaliza changamoto hii. Wananchi waelimishwe juu ya gharama za ufungaji wa maji na gharama za kulipia. Tofauti na hapo hii Bodi ya Maji hapa hatutoelewana hatua za kinidhamu zitachukuliwa endapo wananchi wetu wataendelea kulalamika," Amesema Kunambi.

Mbunge Kunambi amefanya ziara katika Kata ya Mngeta na kuzungumza na Wananchi wa vijiji vya Ikule na Mkangawalo ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye kata hiyo pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zao.





Share To:

Post A Comment: