MBUNGE wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi ameendelea na ziara yake katika jimbo hilo ambapo amekagua ujenzi wa daraja la kuduma la Luipa linalogharimu kiasi cha Sh Bilioni 1.2 ambalo litahudumia wananchi wa kata nne.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mbunge Kunambi amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ili wananchi wa kata hizo nne za Mbingu, Igima, Mofu na Namawala waweze kunufaika nalo.

" Tunaishukuru Serikali yetu ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujali maslahi ya wananchi wa Jimbo letu la Mlimba, kwa muda mrefu tumekua tukiteseka na kivuko hiki lakini kukamilika kwake sasa kutaenda kumaliza kabisa kero iliyokua ikitukabili.

Nitoe rai kwa mkandarasi anayetekeleza ujenzi huu kukamilisha kwa wakati ili sasa wananchi wetu waweze kulitumia na kuepusha vifo vya watu wetu hasa nyakati za mvua ambapo ilikua inashindikana kupitika kutokana na daraja la mbao lililokuepo kuzidiwa.

Lakini pia daraja hili litaboresha maisha ya wananchi wetu kiuchumi kwani sasa wataweza kusafirisha mazao yao bila changamoto yoyote ile. Niendelee pia kutoa wito kwa wakandarasi kuhakikisha pia wanapotekeleza miradi hii wanatoa ajira kwa vijana wetu wa eneo husika," Mbunge Kunambi.

Baada ya kukagua mradi huo Mbunge Kunambi pia alifanya mkutano na wananchi wa Kata ya Mbingu na kueleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo na jimbo la Mlimba kwa ujumla pamoja na kutatua papo kwa hapo kero mbalimbali.

Share To:

Post A Comment: