MBUNGE wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi ameendelea na ziara yake katika jimbo hilo ambapo amekagua ujenzi wa mradi mkubwa maji katika kata ya Chisano ukaohudumia kata nne za jimbo hilo na vijiji 12 na ambao unagharimu Sh Bilioni 7.4.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Chisano mara baada ya kukagua ujenzi huo, Kunambi amesema mradi huo ni kielelezo cha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwatua ndoo kichwani wakina mama wa Jimbo la Mlimba.
" Huu ni mradi mkubwa sana katika jimbo letu. Ni mradi ambao unakwenda kumaliza changamoto ya maji katika kata zetu nne za Chisano, Kalengakelu, Mlimba na Kamwene pamoja na vijiji vyake 12. Tuna kila sababu ya kumshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwetu wananchi wa Mlimba.
Nitoe rai kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi huu kutambua kwamba ni kiu yetu wananchi wa kata hizi nne kuona tunapata maji hivyo wakamilishe mradi huu kama ambavyo walisaini kwenye mkataba, ili wananchi sasa waepukane na changamoto za kutembea umbali mrefu kufuata maji," Amesema Kunambi.
Aidha Mbunge huyo amefika katika kata ya Masagati na Utengule ambapo amefanya mikutano ya hadhara ya kuzungumza na wananchi kuwaeleza utekelezaji wa ilani pamoja na kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.
Pia Kunambi amekagua madarasa yanayojengwa katika Shule ya Msingi Ibako iliyopo katika Kata ya Masagati na kueleza kuridhishwa na usimamizi wa ujenzi huo ambao unakwenda kumaliza changamoto ya madarasa kwenye shule hiyo.
Post A Comment: