Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeishauri Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuishirikisha Sekta binafsi katika utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kukuza utalii ili kufikia lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) katika kikao cha kupokea taarifa za Utekelezaji wa Majukumu mbalimbali za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) na Idara ya Utalii katika ukumbi wa Utawala Annex Bungeni jijini Dodoma leo.
"Sekta binafsi ni muhimu sana katika mafanikio ya sekta ya utalii na inasaidia sana kwenye kukua kwa sekta ya utalii" Mhe. Mnzava amesisitiza.
Amesema kupitia kikao hicho Kamati imejifunza kwamba kuna umuhimu sana wa Serikali kukutana mara kwa mara na wadau wake na hivyo kuiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kutoa nafasi kwa wadau kwa kusikiliza changamoto zao na kushirikiana nao kuzitatua.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuweka mfumo wa uuzaji wa vitalu vya uwindaji wa kieletroniki kwa kuwa umeongeza ufanisi na kupunguza urasimu.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema Wizara itafanyia kazi mapendekezo ya Kamati na pia itaendelea kushirikiana na wadau.
Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na wadau wa kutoka Chama cha Waongoza Watalii nchini (TTGA), Chama cha Wawindaji wa Kitalii(TAHOA) na Wafanyabiashara ya Nyara za Wanyamapori ( TWEA).
Post A Comment: