Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameitaka Kampuni ya uchimbaji wa Kati wa Makaa ya Mawe ya Edenville Tanzania Limited kuchangia huduma kwa jamii inayozunguka eneo la shughuli za uchimbaji wa madini hayo kama Kanuni chini ya Kifungu namba 129 cha Sheria ya Madini kinavyoelekeza.

Hayo, ameyasema wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Pande Kijiji cha Komolo wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa kwenye mkutano wa hadhara ambapo amesisitiza kampuni hiyo kuwasilisha Mpango wa Wajibu wa Mmiliki wa Leseni ya Madini kwa Jamii inayozunguka Mgodi.

"Naomba mkutane na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ili kupata vipaumbele vya eneo husika ili mjue mnatakiwa kuchangia katika maeneo gani, uchangiaji huo sio ombi bali ni takwa la kisheria kwa mmiliki wa leseni kuchangia huduma za kijamii inayozunguka mgodi", amesema Dkt. Kiruswa.

Aidha, Dkt. Kiruswa ameliagiza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuitembelea Kampuni ya Edenville Tanzania Limited ili kuona namna bora ya kushirikiana nayo kwa lengo la kusaidia na kuongeza tija kwenye uzalishaji wa madini hayo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameitaka Kampuni ya Edenville Tanzania Limited inayomilki hisa kwa asilimia 90 kuachana na migogoro na mbia mwenza mwenye hisa ya asilimia 10 ambapo amewataka kufanya kazi kwa ushirikiano na kila mmoja kupatiwa haki yake kwa mujibu wa mkataba waliyowekeana.

Awali, Dkt. Kiruswa alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa lengo la kupata taarifa za shughuli za Sekta ya Madini zinazoendelea kufanyika Mkoani humo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kufanya ziara katika mkoa huo na kumuomba kuwapa moyo wachimbaji wa madini ili kuchochea maendeleo ya sekta hiyo.

Baadhi ya viongozi walioshiriki ziara hiyo ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali, Mwakilishi wa Kamishna wa Madini Mhandisi Shija Itandiko, Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Rukwa Masia Gabril, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini wa Mkoa wa Rukwa Masie Mambegele na Meneja Kampuni ya Edenville Tanzania Limited inayomilki mgodi wa Makaa ya Mawe Darwesh Gamdust.

Share To:

Post A Comment: