...............................................
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Temeke, Mobhare Matinyi,
amewaagiza vijana saba wazalendo waliondoka Dar es Salaam leo asubuhi kuanza
matembezi ya mikoa 16 kuzitangaza kazi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akiwakabidhi bendera ofisini kwake, DC Matinyi
alizitaja baadhi ya kazi zilizofanywa wilayani Temeke mwaka 2022/23 na thamani
ya fedha zilizotolewa na Rais Samia kuwa ni pamoja na miradi ya afya sh.
bilioni6.1, elimu ya msingi sh. bilioni 7.6, elimu ya sekondari sh. bilioni 10,
maji sh. bilioni 15.5, umeme sh. bilioni 61.6 na barabara sh. bilioni 43.7.
Alisema kwa ujumla wilaya ya Temeke ilipatiwa na
Rais Samia zaidi sh. bilioni 152 katika kipindi hicho kutokana na wingi wa
wakaazi wake ambao wanafikia milioni 1.35 na nia yake ya kuleta maendeleo kwa
Watanzania. Aliwaambia vijana hao kuwa katika kilomita 3,624 wanazotarajia
kutembea kwa miguu watakutana na ushahidi lukuki wa kazi za Rais Samia.
Vijana hao saba wanaoongozwa na Abiudi Maugo
wanatarajiwa kuhitimisha matembezi yao mkoani Manyara wakati wa sherehe za
kuuzima mwenge hapo Oktoba 14, 2023.
Vijana wengine ni Sophia Kooni, Beatrice Masanja, Shabani Juma, Jesca Giribert, Flora Erenest na Paul Mkinga. Hii ni mara ya nane kwa vijana wa Temeke kufanya matembezi nchini kuunga mkono matukio au dhima tofauti.
Post A Comment: