Na John Walter-Babati

Viongozi na Watumishi wa Umma wilaya ya Babati wameagizwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maadili ya uongozi kulinda hadhi na haiba ya Serikali mbele ya umma.

Hayo yameelezwa na mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange wakati akisuluhisha mgogoro uliopo kati ya mtendaji wa kijiji cha Secheda na Mtendaji wa Kijiji hicho waliopishana kauli na kusababisha kuchanika kwa hati ya kukamatwa mtuhumiwa.

Twange amesema Viongozi wote kuanzia ngazi ya kitongoji wanafanya kazi kwa niaba ya Rais, hivyo kwenda kinyume ni kudhalilisha mamlaka hiyo ya juu na wananchi kukosa imani.

"Viongozi mkianza kugombana, mtashindwa kufanya kazi na kuchelewesha miradi ya maendeleo"

Amesema Uongozi mzuri ni ule unaojali na kuweka mbele maslahi ya umma, na  sio tu huongeza tija kiutendaji, bali pia huleta maendeleo endelevu ya wilaya,mkoa na hata taifa kwa ujumla.

“Tunahitaji viongozi na watendaji waadilifu kusimamia miradi iliyopo ikamilike kwa wakati,  lazima tutambue kuwa vyeo, madaraka na utendaji wetu hutoa taswira ya Serikali, tusilewe madaraka,” amesema Twange

Wajumbe wa Kijiji cha Secheda wanadai kuwa siku ya Jumamosi Agosti 5,2023 wakiwa kwenye kikao mtendaji wa kijiji alitaka kumwadabisha mmoja wa wananchi anayehamasisha mgomo kwa wenzake wanaofanya shughuli ya ujenzi katika shule mpya ya Sekondari Secheda ambapo aliandika hati ya kukamatwa kwa kijana huyo na mwenyekiti kuonekana kuchukizwa na jambo hilo na kuamua kuichana hati hiyo.

Baadhi yao wanadai kuwa sio mara yake ya kwanza kufanya vitendo hivyo, kwani alishawahi kuwachapa wataalamu wa maji waliokuwa wakitimiza majukumu yao kijijini hapo.

Hata  hivyo baada ya Mwenyekiti Gabriel Ingi kupishana na mtendaji wa Kijiji Magete Tika, Mamlaka katika halmashauri ya wilaya ya Babati ilimuamishia Mtendaji katika kijiji jirani cha Luxamanda kuendelea na majukumu yake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Luxmanda Petro Mogitu akizungumza jambo katika kikao maalum kilichoitishwa na mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange.




Hapa mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange akisisitiza Jambo wakati akiongea na wajumbe wa kijiji cha Luxmanda.

Share To:

Post A Comment: