Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Daniel Chongolo amewataka Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kuongeza juhudi katika kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Ndugu, Chongolo amesema hayo leo Mkoani Arusha aliposhiriki Kikao Kazi cha Mafunzo ya kuwajengea uwezo Viongozi wa Mkoa wa Arusha kinachoendelea katika Hotel ya The Retreat At Ngorongoro-Karatu ambapo pamoja na mambo mengine amesema Serikali inayoongozwa na CCM imekuwa ikipelekeka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa Wananchi lakini bado kuna changamoto kubwa kwani kuna baadhi ya maeneo Vitengo hivyo havitumiki ipasavyo kwaajili ya kutangaza mafanikio hayo.

"CCM ndiyo yenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-25 na katika Ilani yetu tumeeleza bayana mambo mbalimbali tutakayoyatekeleza kwa Wananchi hivyo ni Jukumu la kila Kiongozi katika ngazi zote husika kuelezea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Uongozi mahiri wa Rais Samia kupitia Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini,tunataka kuona Wananchi wanapata taarifa sahihi za miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ".alisema Chongolo

Amesema Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini vikitumika ipasavyo vitasaidia kuonyesha namna gani Serikali inavyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ambayo ni Miradi mbalimbali ya maendeleo iliyohaidi wakati wa Uchaguzi hivyo kusaidia kuwapa uelewa mpana Wananchi wa kujua namna Ilani ya Uchaguzi inavyotekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya sita akitolea mfano wa Miradi ya Elimu, Afya, Maji na barabara inayoendelea Nchi nzima.

Sambamba na hilo amesema Viongozi wengi wamekuwa wepesi kukimbilia Vyombo vya Habari kuelezea kero za maeneo wanayoyaongoza, lakini Serikali inapotatua kero hizo wamekuwa wazito kutumia Vyombo vya Habari au Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini kuelezea namna Serikali ilivyotatua kero hiyo ili Watanzania waelewe.

Aidha,ndugu Chongolo amesema kuwa Maafisa Mawasiliano Serikalini wanatakiwa kuongeza ubunifu katika utendaji kazi wao kwa kuhakikisha wanayaelewa vyema maeneo wanayoyafanyia kazi pamoja na kuitumia ipasavyo mitandao ya kijamii ili kuendelea kuhabarisha umma juu ya wapi tulipotoka,wapi tulipo na wapi tunakoelekea kama Nchi.





Share To:

Post A Comment: