Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema ni marufuku
wananchi kutozwa fedha wakati wa kipimo cha malaria cha haraka, dawa za Alu, dawa
za SP kwa wajawazito pamoja na sindano ya malaria kali.
Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa
Wilaya ya Kishapu ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili ambayo imelenga
kutembelea na kukagua utoaji wa huduma za Afya Mkoani Shinyanga.
Waziri Mhe. Ummy amesisitiza huduma ya kipimo cha haraka
cha malaria ile ya kudungwa sindano, dawa za Alu, dawa za SP kwa wajawazito
pamoja na sindano ya malaria kali zifanyike bure isipokuwa kipimo cha BS.
“Kipimo
cha Malaria cha haraka kile unadungwa sindano ni bure usilipie hata shilingi ukiombwa
hela nipigie simu lakini pia dawa ya Malaria SP
bure, dawa ya Malaria Alu ni bule na sindano ya Malaria kali bure mganga
mkuu wa wilaya nataka usimamia maelekezo ya serikali dawa hizo zitolewe bure
lakini mwananchi ukiambiwa kile kipimo cha BS kile ndiyo unaweza kulipia”.amesema
Waziri Ummy
Waziri Ummy amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya
Kishapu kuwa serikali itaendelea kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya Afya ikiwemo uhaba wa watumishi,
ubovu wa miundombinu pamoja na magari ya
kusafirisha wagonjwa (Ambulace).
Aidha Waziri huyo amewataka wataalam wa Afya wakiwemo madaktari
na wauguzi Mkoani Shinyanga, kuzingatia weledi na uadilifu katika utoaji wa
huduma bora kwa wananchi hasa wagonjwa.
Amesema ni muhimu ufanyike uchambuzi kwa Kila
Halmashauri ili kubaini kada zinazokwamisha upatikanaji wa huduma za Afya
katika Mkoa wa Shinyanga.
Awali wakati akizungumza mbunge wa jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi.
Mhe. Butondo
amesema pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali katika sekta ya
Afya, zipo baadhi ya changamoto zinazowakabili wakazi wa Kishapu ikiwemo uhaba
wa watumishi pamoja na magari ya kusafirishia wagonjwa (Abulace).
Katika taarifa yake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph
Mkude amesema taratibu za kuzuia mianya ya uharifu ikiwemo wizi zinaendelea
kuzingatiwa ambapo amemhakikishia waziri Ummy kuwa ataendelea kuimarisha ulinzi
na usalama katika sekta ya Afya Wilaya ya Kishapu.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Shinyanga wameipongeza
serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya ambapo wamemuomba waziri wa
Afya kushughulikia haraka changamoto zilizopo.
Waziri wa Afya Mhe.Ummy
Mwalimu Julai 14, 2023 amehitimisha ziara yake ya siku mbili Mkoani
Shinyanga ambapo katika wilaya ya kishapu ametembelea na kukagua utoaji wa
huduma za Afya Hospitali ya Wilaya ya Kishapu ambayo inaitwa Jakaya Mrisho
Kikwete, Kituo cha Afya Negezi pamoja na Zahanati ya Maganzo.
Post A Comment: