WATU 86 MKOANI TANGA KUFANYIWA UPASUAJI WA KUREKEBISHA VIUNGO
Na. Mwandishi Wetu, Tanga.
Jumla ya watu 86 Mkoani Tanga wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha viungo na kati yao 43 washafanyiwa chini ya Kambi maalum ya Upasuaji wa Viungo (Reconstructive & Cosmetic Surgery) inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tanga (Bombo).
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu mara baada ya kutembelea Kambi maalum ya upasuaji wa kurebisha viungo (Reconstructive & Cosmetic Surgery) inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tanga (Bombo) mkoani humo.
Waziri Ummy ameeleza kuwa upasuaji huo unaofanywa na madaktari bingwa kutoka Ujerumani na Tanzania sio kama ule wa 'wadada' wa kisasa bali ni upasuaji wa Viungo ili kuvirejesha katika utendaji wake wa kawaida.
Waziri huyo ameshuhudia wagonjwa ambao wamekatwa miguu yote miwili (baada ya kupata ajali au maambukizi yaliyopelekea kukatwa miguu) sasa wanatembea kwa miguu bila fimbo au msaada wowote baada ya kuwekewa 'miguu', ambapo amesema hakika ni jambo la kutia faraja na kuendelezwa.
“Kipekee, ninamshukuru sana Professor Juergen Dolderer na Taasisi yake ya Interplast German na University Medical Centre, Bayreuth German kwa kuichagua Hospitali yetu ya Bombo kuwa mshirika wa kutoa huduma hizi hapa nchini ikiwemo kuwajengea uwezo wataalam wetu wa kitanzania kufanya upasuaji wa kurekebisha viungo”, amemshukuru Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema mahusiano ya Tanga na Ujerumani ni ya kihistoria na inasadikika kuwa Bombo ndio Hospitali ya kwanza kujengwa na Wajerumani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Amewashukuru Interplast kwa kukubali ombi lake la kuifanya Bombo Hospitali kuwa Kituo cha Umahiri cha Upasuaji wa Viungo (Centre of Excellence on Reconstructive and Cosmetic Surgery) ukanda wa Afrika Mashariki hivyo wanakamilisha taratibu zote zinazohitajika ili kuyapa nguvu maono haya.
Waziri Ummy amesema kuwa Kambi maalum ya upasuaji wa kurekebisha viungo (Reconstructive & Cosmetic Surgery) inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tanga (Bombo) ilianza Tarehe 17 Julai 2023 hadi leo na Kambi itafungwa tar 28 Julai mwaka huu.
Post A Comment: