WAKINA MAMA 98 WAPONA SARATANI YA SHINGO YA MLANGO WA KIZAZI TANZANIA


Na. Said Nyaoza

Serikali imesema NBC Marathon Dodoma ndani ya miaka mitatu imefanikisha wakina mama 1,300 waliokuwa na Saratani ya Mlango wa kizazi kuanza kupatiwa matibabu katika Taasisi ya Ocean Road iliyopo Jijini Dar Es Salaam na kati ya hao 98 wamesha pona na kuruhusiwa kurejea majumbani mwao.


Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa leo katika mbio za NBC Dodoma Marathon 2023 katika Uwanja wa Jamhuri Mkoani Dodoma.


 Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopira kupitia mbio za NBC Marathon Dodoma zimefanikisha kukusanya zaidi ya shilingi Milioni 500 na tayari zimesaidia wakina mama 23,000 kupata vipimo mbalimbali vya Afya ya Uzazi


"Hili ni jambo la faraja sana kwa nchi yetu kwa kuwa maeneo mliyo yachagua ili kuelekeza mapato ya mbio hizi ni ya muhimu sana ni kweli kwamba saratani ya shingo ya mlango wa kizazi kwa wakina mama imekuwa ikigharimu maisha ya wengi kuliko saratani zingine zote”, amesema Mhe. Majaliwa 


Amesisitiza kuwa vifo vingi vinaweza kuepukwa iwapo tutaongeza ufahamu, elimu ya kujikinga na kuhamasisha umuhimu wa kuwahi tiba kabla ya kuumwa.


Mhe. Majaliwa amesema Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassani inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kuhakikisha kunakuwa na ustawi wa afya ya mama na mtoto ikiwemo mpango wa Mama Samia Mentorship Program.


Amesema kuwa mpango huo ni mahsusi kwa mafunzo ya muda mfupi kazini kwa madaktari bingwa na wakunga ili waweze kuimarisha utoaji huduma kwenye Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya.



Mhe. Majaliwa amesema kuwa mpango mwingine wa Serikali ni kuongeza wigo wa kutoa huduma za kupima dalili za awali za saratani ya uzazi kutoka Vituo vya Afya 925 vilivyopo hadi kufikia vituo vya Afya 1,025 hapa nchini.


“Mwingine ni kuimarisha wigo wa kutoa huduma za watoto wachanga kwa ujenzi wa wodi maalum, kununua vifaa tiba na mafunzo kwa watumishi kutoka hospitali 175 hadi kufikia hospitali 275 katika mwaka 2023/2024”ameeleza Mhe. Majali.


Mhe. Majaliwa amesema katika mbio za NBC Marathon mwaka 2023 inakadiria kukusanya zaidi ya shilingi Milioni 300 ambapo zinatarajiwa pia kutumika katika kuboresha Afya ya Mama na Mtoto.


"Fedha hizo zinatarajia kutumika katika maeneo makuu mawili, kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya mlango wa kizazi kwa wakina mama na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa taaluma ya ukunga nchini ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi" amebainisha Mhe. Majaliwa 


Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2021 mpaka sasa takribani wanawake 40,000 walifikiwa na huduma ya mkoba ambazo zinajumuisha huduma za elimu, uchunguzi wa awali, rufaa na matibabu ya saratani kupitia programu maalumu inayojulikana kama ‘Samia Suluhu Hassan Outreach Program’



Aidha Prof. Nagu ametoa rai kwa watanzania kuzingatia mtindo Bora wa Maisha ili kujikinga na Magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya saratani na kuwaasa wanawake kupima saratani ya mlango wa kizazi kwani endapo itagundulika mapema, Saratani ya Mlango wa Kizazi inatibika na kupona. 


"Naomba nitumie jukwaa hili kuwaasa wanawake wote nchini kujitokeza kupima saratani ya mlango wa kizazi ambapo tuna jumla ya vituo 925 nchi nzima vyenye uwezo wa kutoa huduma hii ili kuwafikia wakina mama nchini." Ametoa wito Prof Nagu






Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: