WAKATI mjadala kuhusu uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam ukiendelea, Taifa halina budi kufanya uamuzi wa kuiboresha sasa au kuiacha ipoteze umuhimu wake kutokana na ushindani unaoikabili.
Pamoja na nafasi yake kijiografia kukaa kimkakati na kuipa manufaa ya kuhudumia kwa urahisi nchi sita za Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda na Uganda inazopakana nazo zisizokuwa na bandari, kukosekana kwa ufanisi katika bandari hiyo kunaifanya nafasi hiyo kutokuwa na faida tarajiwa za kiuchumi kwa taifa na kuwapa washindani wake, bandari za Mombasa, Kenya na Lobito nchini Angola, nafasi ya kuinyang'anya wateja.
Januari 27, 2023 mawaziri wa usafirishaji wa Angola, DRC, na Zambia kwa msaada na uratibu wa sekretarieti ya SADC walitia saini makubaliano ya kuendeleza ushoroba wa Lobito yaani Lobito Corridor Transit Transport Facilitation Agency (LCTTFA).
Ushoroba wa Lobito unaanzia Bandari ya Lobito kwenye Bahari ya Atlantic unaambaa kutoka magharibi kuelekea mashariki kupitia majimbo ya Benguela, Huambo, Bie’ na Moxico na kupitia katika maeneo ya uchimbaji madini katika jimbo la Katanga nchini DRC na ukanda wa shaba nchini Zambia.
Utekelezaji wa makubaliano haya utarahisisha ukuaji wa biashara za ndani na miongoni mwa nchi hizo kwa sababu unazipa Zambia na DRC njia mbadala ya kimkakati na fupi inayounganisha majimbo ya uchimbaji madini kwa nchi hizo na bahari kupitia bandari ya Lobito.
Angola kwenye ushoroba huo unaunganisha zaidi ya asilimia 40 ya watu wake na maeneo ya uwekezaji mkubwa katika kilimo cha biashara kwenye majimbo unamopita.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia zinamiliki asilimia 34 ya madini ya cobalt duniani na zaidi ya asilimia 10 ya madini ya shaba, ambazo husafirishwa ama kupitia Bandari ya Dar es Salaam au Durban, Afrika Kusini.
Kama mwenendo wa utendaji kwenye bandari yetu utaendelea hivi upo uwezekano mkubwa wa Bandari ya Dar es Salaam kupoteza soko la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia na kuchukuliwa na Bandari ya Lobito.
Huku ushindani dhidi ya Bandari ya Dar es Salaam ukiongezeka kwa majirani zake wa SADC, hali ni hiyo hiyo kwa Afrika Mashariki, tayari Kenya wametangaza kutafuta mbia wa kuwekeza katika bandari ya Mombasa ili kuongeza ufanisi.
Mfanyabiashara na mdau wa masuala ya bandari na usafirishaji wa meli na malori, anasema kuwa kampuni ya DP World ina uwezo wa kipekee wa kuleta mageuzi ya kiuchumi Tanzania kutokana na mtandao wake mpana wa kimataifa kwenye mabara yote duniani na utakaofanikisha kuleta shehena kubwa na meli nyingi kwenye bandari ya Dar es Salaam na kuwezesha kuhimili ushindani.
“Katika mazingira haya ni wazi kuwa uamuzi wa kuboresha utendaji kazi katika bandari ya Dar es Salaam ni lazima ufanyike sasa tukichelewa tutakuta mwana si wetu,” anasema.
Uwekezaji wa DP World katika bandari ya Dar es Salaam, pamoja na kuifanya ikabili vyema ushindani huo kutoka bandari za Lobito na Mombasa, utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa lenyewe na wananchi wake kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, uwekezaji wa DP World utakuwa na manufaa makubwa na mengi ikiwemo kuongeza pato la serikali kutoka Sh. trilioni 7.76 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh. trilioni 26.7 kwa mwaka ifikapo mwaka 2032/2033. Kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kwenye bandari ya Dar es Salaam kutoka tani milioni 18.4 kwa mwaka 2021/2023 hadi tani milioni 47.5 kwa mwaka ifikapo 2032/2033.
“Kutakuwa na ongezeka kwa meli zinazotia nanga bandarini kutoka meli 1,569 kwa mwaka hadi meli 2,950 kwa mwaka ifikapo 2032/2033, itaongeza ajira kutoka 28,990 kwa mwaka hadi kufikia ajira 71,907 kwa mwaka 2032/2033.
Miaka kumi iliyopita Mei 21, 2013 mchumi mwandamizi wa Benki ya Dunia, Jacques Morisset, katika makala yenye kichwa cha habari, “If had three minutes with President Jakaya Kikwete” (Kama nikipata dakika tatu na Rais Jakaya Kikwete) iliyochapishwa katika jarida la Africa can end poverty, anasema pamoja Tanzania kuwa na matatizo mengi ya kiuchumi, angetumia muda huo kumweleza umuhimu wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam.
“Bandari ina nafasi muhimu kwa nchi yake. Bandari inahudumia asilimia 90 ya biashara ya nje ya Tanzania na ni lango la kimkakati kwa biashara ya kimataifa kwa nchi sita inazopakana nazo zisizo na bahari. Nitamwambia kuwa karibu raia wote na kampuni zinazofanya kazi Tanzania zinaathirika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa utendaji wa bandari hii.”
Anaeleza kuwa watoto wagonjwa walioko hospitali, wanaposubiri dawa za kuwatibu zinaweza kukwama bandarini, kama wakulima wanalalamikia kupanda kwa bei ya mbolea hii kwa sehemu ni kutokana na ucheleweshaji wa shehena bandarini.
Mtaalamu huyo wa uchumi anaeleza kuwa bandari ya Dar es Salaam haiusaidii uchumi wa Tanzania kwa kiwango kinachotakiwa kutokana na matatizo kukosa ufanisi yanayosababisha ucheleweshaji wa shehena, rushwa, kuongeza gharama za usafirishaji ambazo mzigo anaubeba mlaji wa mwisho kwenye bei za bidhaa.
“Uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam una nia ya kuongeza ufanisi katika bandari yetu ili iweze kishindana na bandari zingine ambazo zinatishia kupokonya biashara yetu,” alieleza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia uchukuzi, Dk. Ally Possi, katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari.
Tangu serikali itie saini makubaliano ya kiserikali na Dubai kwa ajili ya uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam, kumekuwa na mjadala miongoni mwa jamii kuhusu namna Tanzania itakavyonufaika na uwekezaji huo, huku serikali kupitia viongozi wake mbalimbali ikisisitiza kuwa maslahi ya taifa yatazingatiwa kikamilifu.
Post A Comment: