Na; Elizabeth Paulo, Dodoma

Mikoa ya Dodoma na Singida imeendelea kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao ya kilimo mifugo na uvuvi. 


Kutokana na Kuathirika huko Mikoa hiyo Imepanga Maonesho ya 88 ya mwaka huu 2023 kutoa ujumbe ambao utawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuhimili mabadiliko hayo.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Rosemary Senyamule amebainisha hayo leo alipofanya Mkutano na waandishi wa Habari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jengo la Mkapa kwa dhumuni la kuukaribisha Umma wa Dodoma, Singida na Watanzania Kushiriki Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini yanayofanyika kila mwaka kuanzia tarehe 01 Agosti na kufikia kilele tarehe 08 Agosti.



"Mbinu tutakazowapa Wakulima, Wafugaji ni pamoja na mbinu za hifadhi ya maji na udogo mashambani zikijumuisha matumizi ya makingamaji, kilimo cha mbegu tisa na jembe la mzambia, kuzalisha mazao yanayotumia maji kwa ufanisi (Mtama na alizeti), uzalishaji wa malisho kwa ajili ya mifugo, hifadhi ya misitu na upandaji wa miti, matumizi ya nishati mbadala (Jua, umeme na gesi) kwa ajili ya kupikia". Amefafanua Senyamule


Amesema katika maonyesho ya mwaka huu Makampuni na watu binafsi wameleta teknolojia bora za ufugaji wa mifugo, mbegu bora za mazao mbalimbali kwa kuzingatia vipaumbele vya mkoa wa Dodoma na Singida.


"Taasisi za utafiti za kilimo, mifugo na uvuvi zinashiriki maonesho hayo kuonesha teknolojia mbalimbali zilizozalishwa kwenye vituo vya utafiti na kuwawezesha wakulima kunufaika na elimu ya uzalishaji bora". Amesema Senyamule



Tofauti na Maonesho ya miaka iliyopita, Mkuu huyo wa Mkoa amesema maonesho ya Nanenane 2023 yatahusisha matukio muhimu na makongamano yanayoongeza wigo wa uzalishaji bora huku Matukio hayo yakiwa ni Pamoja na Kongamano la Tasnia ya Alizeti.


"Mikoa ya Dodoma na Singida ilikabidhiwa jukumu la kuzalisha alizeti kwa wingi ili kupunguza nakisi ya mafuta ya kula nchini hivyo Siku hii yatafanyika Maonesho maalumu ya zao la alizeti na kutanabaisha mnyororo mzima wa tasnia hiyo katika eneo maalumu ndani ya uwanja aidha Kongamano la zao la Mtama Pamoja na Siku Maalumu ya Uhamasishaji uzalishaji kuku wa Kienyeji".Amesema


Kauli mbiu ya Maonesho na Sherehe za Nane Nane Kitaifa kwa mwaka 2023 ni; Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula aidha Kaulimbiu ya Kikanda ni Kilimo ni Biashara, Biashara ni Uwekezaji.




Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: