Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete ameagiza takwimu za utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) ziakisi kila Wilaya na Halmashauri zake ili kupata tathmini sahihi itakayowezesha kuweka mipango itakayowafikia walengwa kwa usahihi.
Aidha ameelekeza TASAF Mkoa kuongea na Halmashauri ziweze kusaidia kubeba ama kuongeza nguvu ya kutenga asilimia fedha kuwezesha wenye uhitaji.
Akizungumza na wakuu wa idara pamoja na watendaji wa TASAF Mkoani Pwani, Ridhiwani alihimiza taarifa zipatikane na kutolewa kwa hali za wilaya ili kufikia malengo ya mradi.
Alielezea malengo ya Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona milango inafunguliwa kwa walengwa ,kwa kubadilisha maisha yao kuwatoa kwenye hali ya umaskini.
"Ziwepo taarifa zinazoakisi takwimu sahihi za wenye mahitaji kwa wilaya zote,hizi taarifa za kutoa kimkoa na wilaya moja moja ,tunakuwa hatupati tathmini kwa usahihi,Hatua hii itasaidia walengwa kujua idadi Yao na kufikiwa ili kutimiza Nia ya Serikali inayoelekeza kuwafikia kaya zenye watu wenye uhitaji ili kuondokana na umaskini na kujijenga kiuchumi kuanzisha miradi "alieleza Ridhiwani.
Ridhiwani alielezea Kuna kila sababu pia ya kuendelea kuwafuatilia walengwa ambao wametolewa ili kujua kama wanaendelea vizuri kwa hali zao za kimaisha na kiuchumi.
"Katika taarifa ya TASAF Mkoani Pwani kulikuwa na walengwa zaidi ya 37,000 na idadi imeshuka kufikia 35,000 ni Lazima hao waliotolewa wafuatiliwe kujua wanaishije unaweza kukuta bado hali ya kiuchumi na maisha yao hairidhishi"
Awali Katibu Tawala mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta alisema , mpango wa kunusuru kaya maskini unatekelezwa katika Halmashauri tisa zenye vijiji 417, hadi kufikia Juni 2023 kaya zinazonufaika na mpango ni 35,427 idadi hiyo imepungua kutoka kaya 37,663 kwa takwimu za mwaka 2020/2021.
Alieleza idadi hiyo imepungua kutokana na kufariki,kuhama,kufutwa katika mfumo na zingine kuhitimu.
Mchatta alifafanua, kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2023 Jumla ya sh Bilioni 14.239.763.7 zimetolewa kwa walengwa.
Nae mratibu wa TASAF Mkoani Pwani,Roselyn Kimaro aliongeza kusema, fedha hizo zimewasaidia walengwa kuongeza kipato cha kaya na kuwezesha upatikanaji wa chakula, huduma za afya na elimu kwa watoto
Alisema, kaya hizo hupokea ruzuku za Msingi na masharti,nyongeza za ujira kwa walengwa wanaoshiriki utekelezaji wa miradi ya ajira za muda (PWP) pamoja na usaidizi wa watu wenye ulemavu
Roselyn alielezea, ipo miradi mbalimbali ambayo wametekeleza kupitia TASAF ikiwemo soko la kisasa Utete,Mochwari Chalinze, Zahanati ya Mwanalugali ambayo ipo hatua ya umaliziaji, Nyumba mbili za watumishi katika Zahanati Vikawe,ufadhili kwa watu wenye ulemavu,sekta ya elimu na miradi ya muda ambapo wananchi wamenufaika kwa kupata ujira.
Post A Comment: