Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa jirani kushiriki hafla ya Maadhimisho ya kumbukizi ya siku ya Mashujaa itakayofanyika Julai 25 mwaka huu katika eneo la kudumu la mashujaa lililopo Mji wa Serikali Mtumba ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wito huo umetolewa leo tarehe 20/07/2023 alipofanya Mkutano na waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jengo la Mkapa kwa dhumuni la kuukaribisha Umma wa Watanzania kushiriki kuwaenzi mashujaa waliolipigania Taifa la Tanzania.
"Julai 25 ya kila mwaka Tanzania huwa inaadhimisha kumbukumbu ya siku ya Mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kuulinda Uhuru wa Nchi yetu. Siku hii ni muhimu kwa sababu inatukumbusha kuhusu wajibu wetu wa kutunza historia ya Mashujaa waliopigania, kutetea na kulinda Uhuru wa Nchi ya Tanzania ili kurithisha vizazi vijavyo umuhimu wa kutumia historia hii kukuza na kuendeleza amani na mshikamano wa kitaifa bila kujali tofauti mbalimbali, ikiwemo za kikabila, kidini na itikadi za kisiasa.
"Ninapenda kuwajulisha kuwa tofauti na ilivyozoeleka katika miaka ya nyuma, ambapo Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa katika Mkoa wa Dodoma yalikuwa yanafanyika katika Viwanja vya Jamatin vilivyopo katikati ya Mji wa Dodoma, mwaka huu (2023) Kilele cha Maadhimisho haya kitafanyika katika Uwanja mpya wa kudumu wa Mashujaa uliopo katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo atakuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama", Mhe. Senyamule
Aidha, shughuli za Mashujaa zitatanguliwa na uwashaji wa Mwenge wa Mashujaa saa 6:00 Usiku wa tarehe 24 Julai, 2023 kuamkia tarehe 25 Julai 202 ambapo Mhe.Senyamule amepewa heshima ya kuuwasha Mwenge huo wa Mashujaa kwa niaba ya Wanadodoma na Mwenge huo utazimwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof. Davis Mwamfupe tarehe 25 Julai 2023 saa 6:00 Usiku.
Tumebakiza takribani siku nne tuadhimishe Siku ya Mashujaa Maandalizi ya Maadhimisho yamekamilika kwa 100% kwaiyo nichukue fursa hii kuwakaribisha Viongozi na Wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na kutoka nje ya Mkoa wa Dodoma, ikiwemo Mikoa jirani ya Singida, Manyara, Iringa na Morogoro kujitokeza kwa wingi kuja kuungana na Wanadodoma katika kuadhimisha siku hii muhimu, ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza katika kiwanja kipya kilichopo eneo la Mtumba".
Hata hivyo Mhe.Senyamule ametumia fursa hiyo kuzishukuru Taasisi zote, ambazo kwa namna moja au nyingine zimeshiriki katika ujenzi wa Mnara Mpya wa Mashujaa katika Mji wa Serikali – Mtumba.
Post A Comment: