Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka ameagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Wanging'ombe kufanya maamuzi juu ya wakandarasi wanaoendelea na ujenzi wa majengo ya shule mpya ya sayansi ya wasichana kwa kushindwa kuendana na kasi ya ujenzi na kusababisha shule hiyo kushindwa kuanza.
Mtaka ametoa maagizo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya shule hiyo yaliyopo katika kijiji cha Usalule ambapo amesema ni fedheha kubwa kwa viongozi kushindwa kusimamia mradi huo ambapo serikali imekwisha toa fedha kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni nne kwa ajili ya ujenzi.
"Mradi huu mheshimiwa Rais alitoa pesa shilingi Bilioni nne kwenye kila mkoa wa Tanzania kwa ajili ya kujenga shule maalum ya wasichana, CMT,Mkurugenzi,kamati ya ulinzi na usalama mkae hapa na mfanye maamuzi leo kama wakandarasi hawa mnaendelea nao au mnavunja hili ni jambo la fedheha,jengo la utawala halijaanza majengo mengine yamechimbwa msingi porojo tu zinapigwa hapa"amesema Mtaka
Awali afisa elimu wa mkoa wa Njombe Nelasi Mulungu ameeleza kuwa fedha takribani shilingi Bilioni tatu za mradi huo zilikwishaingia tangu mwaka 2022 huku Bilioni moja na milioni mia moja ikiingizwa mwaka huu lengo ikiwa ni kuanza kuwapokea wanafunzi wasichana wa kidato cha tano waliokuwa wakitarajiwa kupokewa tarehe 13 mwezi wa 8 mwaka huu lakini serikali imeshindwa kupeleka watoto kutokana na kushindwa kukamilika kwa ujenzi wa madarasa.
Post A Comment: