Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji na biashara na kuhamasisha Taasisi za ndani za fedha kutoa mikopo nafuu na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ili kukuza biashara zao.
Rais Samia amesema hayo wakati akiwasilisha salamu zake kwa njia ya Video kwenye Mkutano wa kwanza wa ngazi za juu wa Maendeleo wa Kimataifa ulioandaliwa na Serikali ya China uliofanyika leo Julai10,2023 Jijini Beijing, China.
Amesema Tanzania kwa sasa inachukua hatua mbalimbali za kuimarisha uchumi ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu, umeme, bandari pamoja na kuipa hadhi Sekta ya Kilimo.
"Ili kufikia malengo yetu kwenye Dunia yenye ushindani mkubwa wa kibiashara hatuna budi kuomba ushirikiano, umoja na ujumuishi kutoka kwenye Taasisisi za kimataifa na tuko tayari na kwa moyo mmoja kuendelea kushirikiana na China pamoja na nchi zote zilizo chini ya Mpango wa Maendeleo Ulimwenguni (GDI) ili kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu ,"amesema.
Mkutano wa kwanza wa ngazi za juu wa Maendeleo wa Kimataifa ulipokea salaam maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa XI Jinping na Wakuu wa Nchi wengine kutoka Solomon Island, Zimbabwe na Pakistan. Mkutano huo umehudhuriwa na ujumbe kutoka nchi 130. Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki.
Post A Comment: