Wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) wakitumia mtumbwi unaotumia injini ya mafuta kusafirishia dawa na vifaa tiba kwenda kwenye vijiji ambavyo vinazungukwa na Ziwa Nyasa wilayani Kyela mkoani Mbeya.
Na Mwandishi Wetu, Kyela
BOHARI ya Dawa (MSD) imeeleza kwamba kwa sasa
imefikia asilimia 95 ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba katika Wilaya ya Kyela
mkoani Mbeya.
Hatua hiyo imefikiwa mbali ya changamoto zilizopo
ikiwemo katika kijiji cha Ikombe ambacho kinazungukwa na Ziwa Nyassa hivyo
kukosa barabara na ziwa linapochafuka dawa na watumishi kuwa hatarini.
Akizungumza wilayani humo Mfamasia wa Wilaya ya
Kyela Emanuel Chacha amesema hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya wilayani
Kyela mkoani Mbeya ni asilimia 95 na wamefikia hali hiyo licha changamoto
zilizopo katika kijiji cha Ikombe kilichopo kisiwani mwa Ziwa Nyasa.
“Tuna vituo 37 vinavyopata dawa na vifaa tiba kwa
mfumo wa kielektroniki wa ELMIS kati ya vituo hivyo vyote vinafikika kasoro
kimoja ambacho kipo kisiwani katika kijiji cha Ikombe kilichozungukwa na Ziwa
Nyasa.
“Kutokana na juhudi za Serikali kituo hicho pia
kinapokea vifaa vya afya kwa asilimia 90 kutoka MSD,”amesema na kutumia nafasi
hiyo kuishukuru Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele
kwa sekta ya afya nchini.
Amesisitiza hatua hiyo ni matokeo ya upatikanaji
wa dawa na vifaa tiba vyenye ubora na kwa wakati na kuboresha huduma kwa
wananchi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya
Ikombe Dk.Joshua Katabazi, amesema ufikishaji wa dawa katika zahanati hiyo
umekuwa na changamoto kutokana na kukosekana kwa barabara na kijiji kuzungukwa
na Ziwa Nyasa.
Ameongeza kituo hicho kinatumia njia ya majini na
kinapokea dawa na vifaa tiba kila mwezi kutoka MSD hivyo upatikanaji wa vifaa
vya afya kuwa wa asilimia 90.
“Kunachangamoto ya usafirishaji wa dawa kutoka
Matema hadi hapa lakini Serikali yetu inahakikisha maboresho sekta ya afya wanakijiji
wa Ikombe wanakuwa wanufaika na sisi watoa huduma tunajivunia wananchi kupata
dawa, vipimo na matibabu yote wanapofika kituoni,”amesema.
Wakati huo huo akizungumza kwa niaba ya wananchi
wa Ikombe Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji Ezekiel Mwamgunda, amesema
wanaishukuru Serikali mbali ya kuwapo kwa changamoto ya kupitisha dawa katika
maji zimekuwa zikifika kwa wakati.
Kuna muda Ziwa linachafuka hivyo kuwa na hatari ya dawa na watumishi wa MSD kuzama ombi langu kwa Serikali kuona haja ya kujenga barabara, mazingira haya ni hatarishi na hali inapokuwa mbaya zaidi inabidi wananchi wajitolee kupita pori kwa pori kufuata dawa kule ng’ambo eneo la Matema,”amesema.
Post A Comment: