Na Damian Kunambi, Njombe.


Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema nwaka huu serikali inatoa kiasi cha sh. Mil. 500 kwaajili ya umaliziaji ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Madilu ambacho wananchi wamejenga kwa asilimia 80 kwa kuchangishana fedha kwa kipindi cha miaka 10.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara alipofanya ziara katika kijiji cha Madilu, Ilawa na Ilininda vilivyopo katika kata hiyo mbunge huyo amesema awali alipata taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi waliodai kuwa kuna fedha ambazo wananchi wamechanga lakini zimeingia mifukoni mwa viongozi ambapo alitoa taarifa katika ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambao walituma wakaguzi watatu ili kuja kufanya uchunguzi.

" Haiwezekani wananchi wanakuwa na moyo wa kuchangia halafu wanatokea watu wasiopenda maendeleo wanatumia fedha ambazo wananchi wamejibana ili wapate maendeleo halafu anatokea mtu anakula, hii ni kuwavunja moyo wananchi". Amesema Kamonga.

Aidha kwa upande wa wananchi wa kata hiyo wamesema kuwa huduma ya kituo cha afya ni kipaumbele kwao kwani wanapata tabu katika kupata huduma na hasa za uzazi kwani wanalazimika kwenda katika kata ya Lugarawa ama Mundindi kitu ambacho kinawalazimu kutembea umbali mrefu sana.

Theodosia Stephano ni miongoni mwa wananchi hao ameishukuru serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaahidi kuwapa fedha hizo kwani zitakwenda kuongeza chachu ya maendeleo ya afya kwa wakazi wa kata hiyo na kuepukana na changamoto wanazozipata hivi sasa katika kupata huduma hiyo.

Aidha kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba amesema serikali ya awamu ya sita inafanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo kwa wananchi sambamba na Mbunge Joseph Kamonga ambaye amekuwa akiwasemea vyema wananchi hao bungeni hivyo kuna kila sababu ya kuwaunga mkono ili maendeleo yaweze kutekelezeka zaidi.

" Nalijua vyema jimbo hili la Ludewa pamoja na changamoto zake, kwakuwa nilishawahi kuwa Mbunge kwa miaka iliyopita ambapo kipindi hicho maendeleo yalikuwa hayafanyiki kwa kiwango hiki kinachofanyika sasa, hivyo tuna kila sababu ya kuwapongeza viongozi wetu hawa maana wanaupiga mwingi" amesema Kolimba.

Share To:

Post A Comment: