Na John Walter-Babati
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini (Mwenyekiti wa kamati ya Bajeti) Daniel Sillo ametimiza ahadi yake ya kukabidhi mashine za kuchapisha katika shule za Sekondari Maganjwa na Arisaayo ili kusaidia katika kuchapa mitihani.
Akizungumza wakati akikabidhi mashine mbili katika shule hizo, amesema kuwa hadi sasa ameshatoa mashine zaidi ya 16 kwenye shule za Sekondari na kwamba hadi mwaka 2025 atakuwa amekamilisha kugawa na kwenye shule za Msingi.
Sillo amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao na atakuwa mstari wa mbele kuwasaidia katika kutatua changamoto zinazo wakabili kwa kadri atakavyoweza.
Katika hatua nyingine, amewapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayofanya ya kufundisha na kuongeza ufaulu katika wilaya ya Babati.
Nao Madiwani wa Kata ya Arri na Dabil wamemshukuru Mbunge huku wakisema kuwa kitendo cha kutoa msaada huo kinaonesha ni jinsi gani anaunga mkono Jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassani ya kujenga miundo mbinu bora ya elimu na kuwezesha wanafunzi kusoma bila shida.
Kwa upande wa wanafunzi wametoa pongezi kwa Mbunge Daniel Sillo kwa moyo alioonyesha kujitoa kuwasaidia kutatua changamoto hiyo na kumuahidi kuwa watasoma kwa bidii na Kufaulu kwa asilimia 100 katika mitihani yao pamoja na kuongeza ufaulu shuleni.
Post A Comment: