Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul, akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi katika ziara yake aliyoianza hivi karibuni jimboni humo.
......................................................
Na Mwandishi Wetu, Babati
MBUNGE wa Jimbo la Babati Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul amewataka wananchi ambao nyumba zao zitapitiwa na ujenzi wa njia ya ‘Bypass’ kuwa watulivu kwani Serikali ipo kwenye mchakato wa kuandaa fidia zao.
Gekul ameyataja maeneo yatakayo athirika na ujenzi huo ni pamoja na Mitaa
ya Hangoni,Kwere,Mrara na Wang'waray.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi ambayo ameianza baada ya vikao vya bunge la bajeti kumalizika hivi karibuni Gekul
amesema kuanzia mwezi wa Septemba waathiriwa wa kupisha ujenzi huo ambao
tayari wamekwisha tambuliwa baada ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)
kufanya tathimini na kupima ujenzi wa barabara hiyo wataanza kulipwa.
Ujenzi wa barabara hiyo ukikamilika utaongeza
pato la ndani la Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwani pia itapita kwenye geti
la kuingia Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Wakati huo huo Mbunge Gekul amewasisitiza wazazi
na walezi kuwapelekea watoto wao shuleni ili baadae waje kuwa watu muhimu
katika familia na Taifa kwa ujumla.
Gekul ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika Shule ya Msingi Ayabadiney iliyopo Kata ya Bonga wilayani Babati.
Post A Comment: