Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amekabidhi mtambo wa kuzalisha umeme jua Sun King Inverter wa 5.1kv wenye thamani ya Mil 7 uliotolewa na Kampuni ya umeme wa sola ya Sun King ambao umesimikwa kwenye jengo la wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
“Nawapongeza sana Kampuni ya Sun King kwa kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia S. Hassan za kuboresha huduma za Afya nchini na hususani huduma inayomlenga mama na mtoto katika mkoa wa Dodoma.
Mtambo huu wa Sun King Inverter ambao mmekabidhi leo utasaidia kuhakikisha huduma ya nishati ya umeme inapatikana muda wote katika jengo hili la huduma ya mama na mtoto.
Tutaendelea kuthamini mchango mkubwa ambao unaofanywa na makampuni binafsi ambayo yamekuwa yakiwekeza kwa ajili ya kuhudumia jamii kama vile kwenye vituo vya afya mashuleni na kwenye sekta ya kilimo na zinginezo.
Nitoe rai kwa makampuni mengine kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za msingi za wananchi kama ambavyo kampuni ya Sun King imefanya”Alisema Mavunde
Naye Mkuu wa Biashara wa Kampuni ya Sun King Tanzania Ndugu Juma Mohamed amesema kampuni yao imejipanga vyema kusaidiana na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za Msingi za Jamii ikiwemo Afya na Elimu kupitia bidhaa mbalimbali wanazozalisha na pia ametoa fursa ya ajira kwa vijana kama mawakala wa bidhaa za sola.
Akitoa shukrani kwa niaba,Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Rufaa Mkoa wa Dodoma Dkt. Peter Mbele amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kuwa bega kwa bega na uongozi wa Hospital katika kuboresha huduma za Afya na kushukuru kipekee kwa kufanikiwa kuipata Kampuni ya Sun King ambapo mtambo wa umeme jua uliofungwa utasaidia kuhakikisha upatikanaji wa umeme katika wodi ya mama na mtoto kwa muda wote na hivyo kurahisisha utoaji huduma.
Post A Comment: