Na. Damian Kunambi, Njombe.
Baada ya kufanyika uzinduzi wa ligi ya Kuambiana Cup katika tarafa ya Masasi wilayani Ludewa mkoani Njombe hatimaye ligi hiyo imezinduliwa tena katika tarafa ya Mawengi huku mgeni rasmi wa uzinduzi huo akiwa ni mkuu wa Wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva.
Akizindua ligi hiyo iliyodhaminiwa na kampuni ya Kuambiana Investment pamoja na banki ya CRDB Mwanziva amempongeza mwanzilishi wa ligi hiyo Imani Haule (Kuambiana) kwa kukumbuka vijana wa nyumbani kwao huku akiwaasa wazawa wengine wa Ludewa waliopo mijini kuja kuwekeza kwenye asili yao.
" Niwaombe wanaludewa wote mliopo mijini kuiga mfano wa mwenzetu Kuambiana maana mnapokumbuka kurejea nyumbani mnachangamsha watu wa kwenu na kuongeza chachu ya maendeleo kwa waliopo huku wilayani", Amesema Meanziva.
Aidha kwa upande wake mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema hii ni mara ya tatu kuhuzuria uzinduzi wa ligi hiyo na mara zote amekuwa akiona mwamko mkubwa wa vijana katika kushiriki ligi hiyo hivyo ni dhahiri kwamba vijana wana uhitaji mkubwa wa uwepo wa michezo mbalimbali.
" Napenda niungane na kauli ya mkuu wa wilaya katika kuwahamasisha wanzetu walio nje ya Ludewa kukumbuka kuleta maendeleo nyumbani, si lazima na wewe uanzishe jambo lako bali unaweza hata kuchangia kwa ambao tayari wameanzisha kama Kuambiana, kuna mwenzetu Ndofi naye ni kiongozi wa Lupingu Day na wengineo pia,"Amesema Kamonga.
Hata hivyo kwa upande wake Mkurugenzi wamashindano hayo Iman Haule amesema lengo la kuanzisha ligi hiyo ambayo hufanyika kila mwaka ni kurudisha furaha nyumbani kwani yeye kama mzawa anaona ana wajibu wa kugawana na wenzake kile ambacho anakipata kwa namna tofauti tofauti ikiwemo kuinua vipaji vya vijana.
Naye meneja wa benki ya CRDB tawi la Ludewa Imani Mwaisango amesema wao ni wadau wa michezo na wamedhamini mashindano hayo kwa kutoa jezi kwa timu zote shiriki ambapo watakuwa sambamba na ligi hiyo hadi mwisho wa mashindano hayo.
Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu na kuhusisha timu 53, ambapo timu 15 kati ya hizo ni za tarafa ya Mawengi, 22 tarafa ya masasi na timu 16 kwa upande wa Ngingama Mkoani Ruvuma.
Post A Comment: