Na Mwandishi Wetu,Mbeya.
Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) imezindua na kutoa elimu ya kilimo bora katika Kituo cha Maarifa cha Yara ambacho kitatumika kama kituo cha mafunzo kwa ajili ya mageuzi ya kilimo.
Kituo cha Maarifa cha Yara kimeanzishwa ndani ya chou kikuu cha sayansi na teknolojia na kitatumika kutoa mafunzo kwa wakulima, wajasiriamali wa biashara ya kilimo, kutoa nafasi za mafunzo kazini na kuelimisha umma kuhusu uendelevu wa kilimo.
Mtaalam kiongozi wa Kilimo wa Yara Tanzania na Rwanda, Bwana Donath Fungu, alisema; "Kituo hichi kitafanya shughuli za kutoa elimu kuhusu lishe kamili ya mazao, afya ya udongo na usimamizi wa mbolea ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima."
Yara ni kampuni kubwa duniani inayozalisha na muuzaji mkubwa wa mbolea bora, virutubisho kamili na linganifu kwa mazao yote nchini na ushirikiano wake na MUST unalenga kuchochea matumizi makubwa na sahihi ya teknolojia ya mbolea na zana za kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo ili kuimarisha ajenda ya kilimo na uendelezaji wa viwanda kitaifa.
“Tumewekeza kwenye kilimo endelevu ili kufikia mapinduzi ya uchumi wa viwanda kwa Taifa ikiwa pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na uzalishaji wa mazao ya kilimo,” amesema bwana Fungu.
Yara Tanzania imeanzisha maeneo ya mashamba darasa ya mahindi, nyanya, na viazi katika chuo Kikuu cha MUST ili kutoa mafunzo ya stadi za vitendo.
"Yara Tanzania itatoa fursa wanafunzi wa vyuo vingine mbalimbali kuja kujifunza kwa vitendo ili kujenga wataalamu mahiri wa kilimo. Kituo cha Maarifa cha Yara pia kitatumika kwa madhumuni ya utafiti wa sayansi mbalimbali za kilimo.
Kwa Upande wake Kaimu Mkuu wa Must, Profesa Godliving Mtui, amesema wameingia makubaliano na kampuni hiyo kwa lengo la kuboresha sekta ya kilimo.
“Tumeingia makubaliano ya mipango mikakati ya kuboresha ushirikiano wa kilimo cha mazao ya nyanya, mahindi na viazi mviringo ikiwepo kufanya utafiti wa kuangalia changamoto kwenye jamii kwa kufanya ubunifu utakaoleta matokeo mazuri,” amesema.
Naye Katibu Tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Mkoa, Said Madito ameitaka Yara kuendelea kufanya utafiti wa udongo na kutoa elimu ya matumizi ya mbolea kwa wakulima.
“Anzisheni vituo vidogo vya kutoa elimu kwa wakulima na kupeleka teknolojia za tafiti za udongo kupitia Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (Must) ambavyo vitaleta tija kubwa katika sekta ya kilimo nchini,” amesema.
Mkulima wa Maharage na viazi mviringo kutoka Wilaya ya Rungwe, Mickdadi Chaula amesema uwepo wa kituo hicho utakuwa fursa kubwa kwao kufika kujifunza teknolijia mbalimbali za kilimo na kuongeza tija katika uzalishaji na kujiongeza kipato.
Post A Comment: