Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga, amewatoa hofu wakulima wa zao la mahindi wilayani Ludewa mkoani Njombe juu ya bei ya zao hilo katika misimu huu kwamba serikali itanunua mahindi hayo kwa bei isiyopungua 700.
Kamonga ameeleza hayo mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kiyombo kata ya Lubonde ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutembelea kijiji kwa kijiji ambapo mpaka sasa tayari amekwisha tembelea vijiji 12 kati ya 77 vya wilaya hiyo.
"Kwa sasa serikali bado ipo kwenye majadiliano juu ya bei ya kununulia mahindi lakini pamoja na majadiliano hayo taarifa za awali ambazo zilitangazwa pia gazetini ni kwamba, bei halisi itakayo tolewa haiwezi pungua sh. 700".
Amesema hivi karibuni alimuomba Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kufika jimboni kwake na kukagua mahindi endapo yamekwisha kauka ili wananchi waanze kuyavuna ambapo imeonekana yamebakiza muda mchache kukauka hivyo yatakapokuwa tayari watafungua vituo vya kununulia mahindi hayo.
Mbunge huyo ameanza ziara hiyo Julai 7 mwaka huu na bado anaendelea nayo ili kuvifikia vijiji vyote 77 vya jimbo hilo ambapo mpaka sasa tayari amekwisha tembelea vijiji 12 ambavyo ni Madilu, Ilawa, Ilininda, Manga, Mfalasi, Iwela, Madope, Mangalanyene, Luvuyo, Masimbwe, Mkiu na Kiyombo.
Post A Comment: