Na. Damian Kunambi, Njombe.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amewataka wananchi wa vijiji vya Mkongobaki, Ugera na Lipangara vilivyopo katika kata ya Mkongobaki wilayani Ludewa mkoani Njombe kuwa wavumilivu na watulivu juu ya mvutano wa eneo linalo stahili kwa ujenzi wa shule ya sekondari uliodumu kwa miaka mingi na kuzidi kuendelea baada ya serikali kutoa fedha za ujenzi hup kiasi cha sh. Mil. 583.
Akizungumza katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika vijiji hivyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutembelea kijiji kwa kijiji ndani ya jimbo hilo kwa lengo la kutoa mrejesho na kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi ambapo mpaka sasa tayari amekwisha tembelea vijiji 36 kati ya 77 vya jimbo hilo.
Kamonga amesema mradi wa ujenzi wa sekondari ni suala la msingi hivyo atarejea tena akiwa na mkuu wa wilaya pamoja na kamati ya siasa ili waweze kukaa kikao cha ndani na wananchi wanaoweza kujenga hoja kisha kuitisha mkutano wa hadhara na kulimaliza jambo hilo.
" Mgogoro huu unaniumiza sana, na ninatani suluhu ipatikane ili muungane kwa pamoja na kuendelea kushirikiana katika kata yenu na kufanya maendeleo", Amesema Kamonga.
Kauli hiyo ya mbunge imekuja baada ya wananchi wa vijiji hivyo kuendelea kutilia mkazo juu ya mvutano huo na kufikia hatua ya wananchi wa kijiji cha Mkongobaki kutoa kauli ya kutaka kuhamia kata ya jirani ya Lugarawa huku wakidai kutojihusisha na shughuli yoyote ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata hiyo.
Alto Bonaventula ni mmoja wa wananchi hao amesema awali wataalamu kutoka wilayani humo walifika na kukagua maeneo yanayostahili kujengwa sekondari hiyo ambapo eneo la Ijenga lililopo katika kijiji hicho ndilo lililoonekana kufaa katika ujenzi huo na huku watu wakilipwa fidia na kisha kuanza kazi kwa hatua za awali ikiwemo ukusanyaji wa mawe.
" Diwani kwa kinywa chake alitusomea barua iliyotoka wilayani ikieleza kuwa eneo hili la kijiji chetu ndilo linafaa sasa tunashangaa kuona baadae wanatuletea mabadiliko kuwa itajengwa makao makuu ya Kata ambako ni katika kijiji cha Ugera kitu ambacho sisi tunaona ni sababu za kisiasa kwani eneo hilo wanalolisema halina vigezo hivyo sisi tumeamua kutoshiriki maendeleo yoyote ya kata hiyo ni heri tushiriki kata ya jirani yetu ambayo ni Lugarawa", Alisema Bonaventula.
Naye Charles Mhagama mkazi wa kijiji cha Ugera amesema wanakijiji cha Mkongobaki hawapaswi kususia maendeleo hayo hivyo wanapaswa kuungana kwa pamoja kwa hiari yao na endapo wataendelea na msimamo wao itatakiwa kutumika njia ya ziada ikiwemo kupatiwa elimu huku John Mwinuka wa kijiji cha Lipangara akiitaka serikali kuwachukulia hatua wanakijiji cha Mkongobaki kwa kususia maendeleo.
Post A Comment: