Na. Damian Kunambi, Njombe.


Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amewataka watendaji wa serikali pamoja na wananchi, kushirikiana katika kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya serikali ili fedha zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ziweze kutumika kwa ufasaha na kuleta matokeo chanya katika maendeleo.

Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo katika mkutano wa kukabidhi msaada wa bati 152 katika shule ya sekondari Madilu huku mgeni rasmi wa makabidhiano hayo akiwa ni waziri wa Sanaa, Utamaduni na michezo Balozi Dkt. Pindi Chana.

Amesema serikali imeleta fedha nyingi za maendeleo katika Wilaya hiyo ikiwemo miradi ya shule, maji, na miundombinu ya barabara hivyo watendaji wa serikali wanapaswa kuwahudumia vyema wananchi pindi wafikapo katika ofisi zao sambamba na kuwashirikisha ujio wa miradi mbalimbali katika maeneo yao na endapo watakuwa na hoja mbalimbali wanapaswa kujibiwa.

" Tukumbuke kuwa sisi watendaji wa serikali ni wauza duka linalomilikiwa na wananchi, hivyo hawa ni waajili wetu! Kwahiyo wanapo tuhoji juu ya bidhaa zinazoingia na kutoka wanapaswa kujibiwa kwa ufasa" amesema Mwanziva.

Aidha pia aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo pindi zinapohitajika nguvu kazi zao kwani shughuli hizo za maendeleo hufanywa kwa kushirikiana na si kusubiri mradi uende vibaya ndipo waanze kutoa kasoro.

"Utakuta mwananchi amejikalisha pembeni hataki kushirikiana na watendaji katika kutekeleza miradi akidai kuwa yeye haimuhusu halafu inapoharibika anakuwa wakwanza kutoa kasoro. Sasa napenda niwaombe ndugu zangu tushirikiane vyema na watendaji hawa ili miradi yetu ikamilike kwa ubora na itusaidie pia" amesema Mwanziva.

Share To:

Post A Comment: